Kamishna Mkuu
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda, ametoa wito
kwa wafanyabiashara wa mitandaoni ambao hawajajisajili na TRA
kujisajili mara moja ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Ameyasema
hayo wakati akizindua rasmi utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano
(MoU) kati ya TRA na Shirika la Kimataifa linashughulika na masuala ya
Kodi (IBFD) ambao umefanyika katika Chuo cha Kodi (ITA) jijini Dar es
Salaam Leo tarehe 24.07.2025.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema
wametoa mwezi mmoja kuanzia Agosti Mosi mpaka Agosti 31.2025
wafanyabiashara wote wanaoendesha shughuli zao mtandaoni wajisajili TRA
ili waanze kuchangia katika kulipa Kodi wakiwemo wenye nyumba
wanaopangisha nyumba zao kutumia Air BNB na hawalipi kodi.
Amesema
watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo la kujisajili ndani ya kipindi cha
mwezi mmoja watachukuliwa hatua ikiwemo kutozwa faini maana
hawajasamehewa kulipa kodi hiyo wakiwemo wale wanaouza vitu mbalimbali
mtandaoni bila kulipa kodi kwani wanavunja sheria kwa kutokulipa kodi
hiyo.
“Kuanzia Agosti Mosi tutakuwa na kampeni kubwa ya
kuhakikisha kila anayefanya biashara ya kupangisha nyumba kupitia
mtandao anasajiliwa na kulipa Kodi pamoja na watu wanaofanya biashara
mtandaoni ambao kipato chao kinazidi Sh. 4,000,000 kwa mwaka nao
watatakiwa kulipa Kodi na kila mmoja atalipa kutokana na kipato chake”
amesema Mwenda.
Kamishna Mkuu Mwenda ametoa wito kwa yeyote
mwenye taarifa za watu wanaofanya biashara mtandaoni kuziwasilisha TRA
na kuwa zipo njia nyingi za kuwabaini watu ambao hawalipi kodi hata kama
wanafanya biashara mtandaoni na risiti zitatolewa kwa njia ya mtandao
kupitia mfumo wa VFD.
Amesema ufuatiliaji wa biashara mtandao
utawezeshwa na mafunzo ambayo watumishi wa TRA wamepatiwa kwa
ushirikiano na IBFD kwa udhamini wa Serikali ya Uholanzi na kubainisha
kuwa makampuni yaliyowekeza nchini na kujihusisha na ukwepaji wa kodi
yatafikiwa.
Mwenda amesema Serikali ya Tanzania imefungua milango
ya uwekezaji ambapo makampuni mengi yanakuja kuwekeza hivyo yanao
wajibu wa kulipa Kodi kwa Mujibu wa sheria.