Halmashauri
ya Wilaya ya Geita imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa
mwaka wa fedha 2024/25 kwa asilimia 125.19 baada ya kukusanya jumla ya
Shilingi bilioni 10.4 dhidi ya bajeti ya awali ya Shilingi bilioni 8.3.
Hii ni zaidi ya Shilingi bilioni 2.1 kutoka makadirio ya awali.
Hatua
hiyo imechangiwa na usimamizi madhubuti wa mapato ya ndani pamoja na
udhibiti wa mianya ya upotevu, ambapo watendaji wa halmashauri waliweka
msukumo mkubwa katika uadilifu na ubunifu wa vyanzo vya mapato.Kupitia
mafanikio ya ukusanyaji wa mapato, Halmashauri iliweza kutenga Shilingi
bilioni 3.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo
katika sekta za elimu, afya, miundombinu na utawala.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa shule mpya, zahanati, vituo vya afya, nyumba za watumishi pamoja na ofisi za kata.
Aidha,
kwa kutekeleza agizo la Serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato ya
ndani kwa ajili ya mikopo, Halmashauri ilitoa mikopo yenye thamani ya
Shilingi bilioni 1.8 kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye
ulemavu waliokidhi vigezo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha
kiuchumi.
Katika kuimarisha mapato ya siku zijazo, Halmashauri imeendelea kutwaa maeneo ya kimkakati kwa ajili ya uwekezaji.
Mnamo
Julai 24, 2025, Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ilifanya ziara
katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro kukagua maeneo yanayotarajiwa
kutwaliwa kwa uwekezaji.
Miongoni mwa maeneo hayo ni eneo lenye
ukubwa wa hekari 14 litakalotumika kwa ujenzi wa kituo cha mabasi
(Katoro Bus Stand) pamoja na soko la Kariakoo Katoro, hatua ambayo
inalenga kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza mapato.
Halmashauri
ya Wilaya ya Geita inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza mapato ya
ndani ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi, huku ikiishukuru
Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuipatia rasilimali na fedha kwa
ajili ya shughuli za maendeleo.