Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali itaendeleza miradi mbalimbali ya kimkakati katika sekta ya nishati ili kuifanya Zanzibar kuwa na umeme wa uhakika.
Ameeleza kuwa hatua hiyo kwa kiasi kikubwa itachochea kasi ya ukuaji wa uchumi, kuboresha huduma za umeme kwa wananchi, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo ya uwekezaji.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 01 Oktoba 2025, alipouzindua mradi wa uboreshaji wa mfumo wa umeme Zanzibar katika hafla iliyofanyika Mtoni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema uzinduzi huo ni ishara na uthibitisho wa nia njema ya Serikali katika utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi, ukiwa pia ni hatua ya kuondoa changamoto za kukatika kwa umeme na tatizo la umeme mdogo katika maeneo mbalimbali, pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji.
Aidha, amesema kuwa Serikali itachukua hatua mahsusi za kujenga miundombinu mipya ya umeme, ikiwemo nishati mbadala kupitia jua na upepo, sambamba na ujenzi wa mitambo ya kusambaza umeme kwa wananchi, kwa lengo la kuhakikisha takribani wananchi 70,000 wanapatiwa huduma hiyo.
Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa katika muda mfupi ujao gharama za kuunganisha umeme majumbani zitashuka kutoka shilingi 200,000 za sasa hadi shilingi 100,000 pekee.
Pia ameweka wazi mikakati mingine ikiwemo kuviunganisha visiwa vidogo vya Njau na Kokota na nishati ya umeme, pamoja na kukamilisha mradi mkubwa wa nyaya za umeme wa chini ya bahari (Submarine Power Cable) kwa ajili ya kupeleka nishati kisiwani Pemba.
Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Wizara ya Maji, Nishati na Madini pamoja na Kampuni ya NOVASIS International kwa usimamizi mzuri na kukamilisha mradi huo kwa wakati, huku akitoa wito wa kutunza miundombinu hiyo ili ilete tija, sambamba na kuendelea kusimamia miradi mingine kwa ukamilifu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Ndg. Joseph Kilangi, amesema mradi huo uliogharimu Dola za Marekani milioni 8.4, na kukamilika kwake kumeiwezesha Zanzibar sasa kupokea umeme kutoka Tanzania Bara kwa kiwango cha 132 KV badala ya 114 KV kilichokuwapo awali.



.jpeg)
