KITUO CHA POLISI CHA MILIONI 700 CHAZINDULIWA RUVUMA

KATIBU mkuu wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi, Aly Senga Gugu, amezindua rasmi kituo kipya na cha kisasa cha polisi cha daraja B Wilaya ya Namtumbo, kilichojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 700. Uzinduzi huo umefanyika tarehe 20 Juni 2025 katika eneo la Namtumbo, mkoani Ruvuma.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu Mkuu Gugu amewataka maafisa wa ukaguzi na askari wa Jeshi la Polisi nchini kote kuendelea kuzingatia misingi na maadili ya jeshi hilo. Ameeleza kuwa upelelezi bora wa mashauri ni msingi muhimu wa haki na utawala wa sheria katika jamii, hivyo ni jukumu la askari kuhakikisha hawawi chanzo cha ucheleweshaji wa mashauri hayo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco Chilya, amesema ujio wa kituo hicho kipya ni faraja kwa jeshi hilo na wakazi wa Namtumbo, kwani awali walilazimika kutumia kituo chakavu na cha kuazima, jambo lililokuwa likihatarisha ufanisi na usalama wa askari na wananchi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Mhe. Bi Ngolo Malenya, amemwomba Katibu Mkuu Gugu kusaidia wilaya hiyo kupata mahabusu, akieleza kuwa kwa sasa watuhumiwa wanaoshtakiwa katika Namtumbo wanalazimika kusafirishwa hadi Songea, hali inayowapa changamoto ndugu wa watuhumiwa hao kufuatilia kesi na kuwaona wapendwa wao.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Contact Form