Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange,
amefanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa
Tanzania - Zambia (TAZA) katika Mkoa wa Iringa na Njombe maneo ya ujenzi
wa njia ya umeme na vituo vya kupoza umeme vya Tagamenda na Kisada.
Katika
ziara hiyo, Bw. Twange alitoa maelekezo kwa wasimamizi wa mradi
kuhakikisha ujenzi wa njia za kusafirisha umeme pamoja na vituo vya
kupokea, kupoza na kusambaza umeme unakamilika kwa wakati kama
ilivyoainishwa kwenye mikataba, huku akisisitiza kuwa usimamizi thabiti
ni muhimu ili kuleta tija na kuhakikisha wananchi wananufaika kwa
wakati.“Simamieni wakandarasi vizuri katika kutekeleza ujenzi wa
miradi hii. Msisimamie kwa mazoea, bali kwa weledi na kasi ili tija ya
miradi hii ionekane na wananchi wapate huduma kwa wakati,” alisisitiza
Bw. Twange.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwapongeza wasimamizi kwa
juhudi zinazofanyika hadi sasa licha ya changamoto zinazojitokeza
katika usimamizi wa miradi mikubwa, aliwataka kuendelea kutumia kipindi
hiki kisicho na mvua kufanya kazi kwa kasi ili mradi ukamilike kwa
ufanisi kama ilivyopangwa na Serikali.
Katika ziara hiyo, Bw.
Twange pia alitembelea miradi ya upanuzi wa vituo vya kupokea na
kusambaza umeme katika Kituo cha Cotex (Iringa) na Kituo cha Makambako
(Njombe), ambavyo tayari vimekamilika kwa kiasi kikubwa na kuanza kutoa
huduma kwa wateja.
Alieleza kuwa hali ya umeme katika mikoa hiyo
sasa imeboreshwa kwa kiwango kikubwa, huku miundombinu ikiwa na uwezo
mkubwa wa kuhudumia mahitaji ya sasa na ya baadaye.
“Nimefurahishwa
na utekelezaji wa miradi hii ya vituo vya kupoza umeme katika mikoa ya
Iringa na Njombe. Kwa sasa tuna uwezo mkubwa wa kuhudumia wateja wengi
zaidi kuliko hapo awali,” alieleza Bw. Twange.