Hospitali ya Rufaa Mtakatifu Joseph Peramiho Yaendesha Kongamano la Kisayansi Kuboresha Huduma za Afya Ruvuma.
Katika
jitihada za kushirikiana na serikali katika kuboresha utoaji wa huduma
bora za afya kwa wananchi, Hospitali ya Rufaa Mtakatifu Joseph Peramiho
iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma, imeandaa
na kuendesha kongamano la kisayansi lililolenga kubadilishana uzoefu wa
kitaaluma katika sekta ya afya.
Kongamano hilo limewakutanisha
waganga wafawidhi kutoka vituo mbalimbali vya afya, hospitali za
serikali pamoja na hospitali binafsi mkoani Ruvuma. Washiriki
wameongozwa na madaktari bingwa kutoka hospitali hiyo, wakiwemo
wataalamu wa magonjwa ya ndani na upasuaji, kwa lengo la kuimarisha
ushirikiano na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa
wananchi, hususan huduma za rufaa.
Akizungumza katika kongamano
hilo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Dkt. Godfrey
Kihaule, pamoja na Mkurugenzi wa Hospitali ya Peramiho, Dkt. Ansgar
Tuffe, walisema kuwa kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu kwa watoa
huduma za afya kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mpya na za
kisasa, ili kuboresha huduma za kinga na tiba kwa wananchi wa mkoa wa
Ruvuma.
Kwa upande wao, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mtakatifu
Joseph Peramiho, Dkt. Deodatus Haule, na Daktari Bingwa wa Upasuaji,
Dkt. Jafeth Mfinanga, walieleza kuwa kupitia kongamano hilo, washiriki
wamepata uelewa mpana kuhusu huduma za kibingwa zinazotolewa hospitalini
hapo. Walisema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi
ya wananchi wanaolazimika kusafiri kwenda mikoa mingine kufuata huduma
hizo.
Kongamano hili ni sehemu ya juhudi za pamoja kati ya sekta
binafsi na ya umma katika kuimarisha mifumo ya afya na kuhakikisha
huduma zinapatikana kwa wakati na kwa ubora unaohitajika.