SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imeendesha mafunzo kwa Maafisa ugani 1701 kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi na jinsi ya kutumia tehama katika kutoa huduma za ugani kupitia mfumo wa M-Kilimo.
Mafunzo
hayo ni ya awamu ya kwanza yalianza tarehe 14 Aprili 2025 na
kuhitimishwa tarehe 20 Juni 2025, na yamesimamiwa na Bi. Paschalina
Hayuma ambaye ni mratibu wa mafunzo kutoka Wizara ya Kilimo, ambapo
amesema kuwa malengo ya mafunzo haya ni kuwafikia Maafisa ugani 4,000
ifikapo 2026/2027.
Aidha amesema kuwa Mfumo wa M-Kilimo
utawawezesha Maafisa Kilimo kuwasiliana na wakulima wengi kwa muda
mfupi, huku wakulima wakipata taarifa mbalimbali zinazohusiana na mazao
na kuwa mfumo huo utasaidia kupata taarifa ya hali ya hewa, ili kulima
kilimo kinacho stahimili mabadiliko ya tabianchi.
Hii ni awamu
ya kwanza ya mafunzo ambayo yamepangwa kutolewa kwa awamu tatu awamu ya
pili itakuwa mwaka wa fedha wa 2025/2026 na awamu ya tatu itakuwa ni
mwaka wa fedha 2026/2027, kupitia utekelezaji wa Program ya Uhimilivu wa
Mifumo ya Chakula Tanzania (TFSRP) unaotekelezwa na Wizara ya Kilimo.
Maafisa
ugani waliokuwa mafunzoni katika vituo vya mafunzo vya MATI Uyole, MATI
Igurusi na MATI Inyala wameshukuru kupata mafunzo hayo na kuahidi
kuyafanyia kazi na kuhakikisha Malengo ya Program ya TFSRP ya kufikia
wakulima 3,000,000 yanafikiwa kama ilivyopangwa kufikia Agenda 10/30.
Tags
Habari