KANISA la Ufufuo na Uzima, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, limeuomba Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kushiriki katika jitihada za kutafuta suluhu ya mvutano unaoendelea kati ya kanisa hilo na mamlaka, ili liweze kurejea katika shughuli zake za kiibada kama kawaida.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
kuwasili katika ofisi za THRDC jijini Dar es Salaam, Askofu Amos Paul,
kwa niaba ya uongozi wa kanisa hilo, alisema kuwa sintofahamu iliyopo
kwa sasa imewalazimu kutafuta msaada wa mtandao huo wa Watetezi wa Haki
ili kuhakikisha Haki yao ya kuabudu inalindwa.
Amesema kuwa hali
hiyo imezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa waumini, hasa kutokana na hatua
zilizochukuliwa na askari polisi kuondoa waumini kwa nguvu na kuzuia
kuendelea kwa ibada katika baadhi ya matawi ya kanisa hilo.
Kwa
upande wake, Wakili Onesmo Olengurumwa, Mratibu Kitaifa wa THRDC, ametoa
wito kwa Waziri wa Mambo ya Ndani pamoja na Jeshi la Polisi kukaa meza
moja na uongozi wa kanisa hilo kwa lengo la kuhitimisha mvutano huo kwa
njia ya mazungumzo ya amani.
Mgogoro kati ya Kanisa la Ufufuo na
Uzima na mamlaka umeibuka kufuatia kile kinachodaiwa kuwa ni ukiukwaji
wa taratibu za usajili na uendeshaji wa taasisi za kidini, madai ambayo
kanisa hilo limekana na kudai kuwa yanatumika kama kisingizio cha
kulizuia kuendesha ibada.
Katika siku za hivi karibuni, askari
polisi walivamia baadhi ya matawi ya kanisa hilo na kuzuia ibada
kuendelea, huku wakiondoa waumini kwa nguvu, hatua iliyozua taharuki na
malalamiko kutoka kwa viongozi wa dini na wanaharakati wa haki za
binadamu.
Tags
Habari