MWANASHERIA MKUU ASHANGAZWA NA "NO REFORM NO ELECTION"

 Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesema anashangazwa na kauli ya “No reforms, no election” ikizingatiwa kuwa mabadiliko ya kisheria yaliyopendekezwa na vyama vya siasa tayari yamefanyika.

Johari ameyasema hayo leo Jumamosi Juni 21, 2025, kwenye kongamano la kwanza la kitaifa la kisheria lililofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam na kubainisha kuwa mageuzi hayo yamefanyika kupitia mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.

Johari ameeleza kuwa mapendekezo hayo yalijumuisha kutungwa kwa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi, kuunganisha sheria ya uchaguzi wa Rais na Serikali za mitaa mchakato uliokamilika mwaka 2024 na kuboresha Sheria ya Vyama vya Siasa kwa kuimarisha ushiriki wa makundi maalumu.

“Yote haya yametekelezwa kutokana na maoni ya vyama vya siasa. Sasa mtu anaposema ‘No reforms, no election’, inashangaza, kwa sababu reforms zimeshafanyika,” amesema Johari kwenye kongamano hilo linaloendelea huku Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete akiwa Mgeni Rasmi.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekuwa kikinadi kampeni yake hiyo ya ‘No reforms, no elections’ nchi nzima kwa takribani miezi minne sasa na kushinikiza kufanyika kwa mabadiliko ya sheria za uchaguzi kabla ya kuelekea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanya Oktoba mwaka huu.



Post a Comment

Previous Post Next Post

Contact Form