Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, imeelekeza wagombea wote wa nafasi ya udiwani waliopitishwa na Kamati za Siasa za Mikoa pamoja na waliokuwa kwenye orodha ya awali, kurejeshwa kwa wapiga kura kwa ajili ya kura za maoni upya.
Maelekezo hayo yametolewa kufuatia kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika Alhamis, Julai 31, 2025, mjini Dodoma, ambacho kilijadili kwa kina malalamiko mbalimbali kuhusu mchakato wa awali wa uteuzi wa wagombea wa nafasi hiyo kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Sekretarieti, hatua hiyo inalenga kuhakikisha haki, usawa na demokrasia vinazingatiwa kikamilifu katika mchakato wa ndani ya Chama.
"Wagombea wote wa udiwani wa kata waliopitishwa na Kamati za Siasa za Mikoa, pamoja na walioko kwenye orodha ya awali waliotumiwa kwa Makatibu wa Mikoa, warejeshwe ili wapigiwe kura za maoni," imesema taarifa hiyo.
Aidha, kikao hicho cha Sekretarieti kimefuta rasmi maelekezo yote yaliyotolewa awali kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi ya udiwani. Makatibu wote wa CCM wa Mikoa wameelekezwa kuhakikisha wanatekeleza maagizo haya mapya kwa ukamilifu na kwa wakati.