Halmshauri ya
Manispaa ya Kigamboni imeyaagiza Makampuni, Taasisi na Wananchi wote
ambao wanamiliki viwanja vya matumizi mbalimbali ndani ya Manispaa ya
kigamboni kuwa wanatakiwa kufanya usafi kwenye viwanja vyao ndani.

ya
siku 7 kuanzia leo August 07,2025 na baada ya siku 7 kupita Manispaa
itafanya ukaguzi na itachukua hatua za kisheria ikiwemo kutoza faini na
kutaifisha viwanja vyote vilivyotelekezwa, huu ukiwa ni utekelezaji wa
agizo la Mkuu wa Wilaya hiyo Dalmia Mikaya (@dalmiamikaya) alilolitoa July 24 , 2025 alipokagua shughuli za usafi katika maeneo mbalimbali ya Kigamboni.
Taarifa
iliyotolewa leo August 07,2025 na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Joseph Semkiwa,
imesema “Baada ya muda huo wa siku 7 kupita Manispaa itafanya ukaguzi na
itachukua hatua za kisheria kwa wale wote ambao hawajavifanyia usafi
viwanja vyao ikiwa ni pamoja na kutoza faini, kufuta umiliki au
kuvitaifisha viwanja vyote vilivyotelekezwa kwa mujibu
wa sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 kifungu cha (44-55), Kigamboni safi ni Mimi na Wewe”
Itakumbukwa
DC Dalmia Mikaya alitoa maagizo kwa Halmashauri hiyo kuhakikisha
inafanya ufuatiliaji kwa Wamiliki wa viwanja na mashamba ili wafanye
usafi ili kupunguza uwingi wa mapori makubwa yanayosababisha Wahalifu
kuyatumia kufanyia uhalifu na pia kuleta mazingira hatarishi kwa
Wananchi.
Akiongea Julai 24, 2025 wakati wa ziara yake ya ukaguzi
katika maeneo ya feri Kigamboni, DC Dalmia alisema ni wajibu wa kila
Mwananchi kutunza mazingira ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko
yanayoweza kuzuilika kwa kufanya usafi wa mara kwa mara huku akiwaonya
pia wanaochafua maeneo ya stendi na wanaogeuza maeneo ya fukwe kuwa
madampo akisema hilo halikubaliki na pia aliagiza daladala zote ziwe na
vindoo vya takataka (dustbin).