Chama
cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimemtangaza rasmi Salum Mwalim Juma
kuwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi
mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.
Tangazo
hilo limetolewa leo katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama hicho
unaoendelea katika Ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam. Mkutano
huo umewakutanisha viongozi wa kitaifa, wajumbe wa chama kutoka mikoa
mbalimbali pamoja na wanachama na wafuasi wa CHAUMMA waliokusanyika kwa
ajili ya kujadili na kuamua juu ya mwelekeo wa chama kuelekea uchaguzi
mkuu wa 2025.
Katika hotuba ya kutangaza uteuzi huo, Mwenyekiti
wa CHAUMMA, alisema kuwa uteuzi wa Salum Mwalim umezingatia rekodi yake
ya kisiasa, uadilifu, maono ya maendeleo, na uwezo wa kuunganisha
Watanzania kutoka makundi mbalimbali.
Aliongeza kuwa chama
kinamwamini Salum Mwalim kuwa ndiye mgombea bora wa kuleta mageuzi ya
kweli ya kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa Tanzania.
Salum Mwalim
Juma, ambaye aliwahi kuwa mwanasiasa kijana mashuhuri na naibu katibu
mkuu wa chama kimoja kikuu cha upinzani kabla ya kujiunga na CHAUMMA,
amekuwa mstari wa mbele katika kupigania haki za wananchi, utawala bora
na uwajibikaji wa viongozi serikalini.