TIRA YAMPA KONGOLE DKT. SAMIA YAJIVUNIA ONGEZEKO LA WANUFAIKA WA BIMA NCHINI

MAMLAKA wa Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), imesema wanufaika wa huduma za bima nchini wameongezeka kutoka milioni 14 mwaka 2021 hadi milioni 25.9,mwaka huu huku hamasa ikiendelea ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika. 
 
Hayo yamebainishwa  Agosti 18,2025 jijini Dar es Salaam na  KAMISHNA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt.Baghayo Saqware wakati wa kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Amesema mali na mitaji katika soko la bima imeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.2 mwaka 2021 hadi trilioni 2.3,mwaka huu.

“Mafanikio haya yanatokana na utekelezaji mzuri wa sera chini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na mafanikio haya yapo kitakwimu zaidi.”

Amesema, pia mafanikio hayo yanatokana na hamasa na elimu inayotolewa na mamlaka kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari nchini.

Vilevile, Dkt.Saqware amesema, idadi ya watoa huduma imeongezeka kutoka 993 mwaka 2021 hadi 2,425 mwaka huu ambapo kuna ongezeko la watoa huduma mpya ikiwemo afya, kidijitali, na bima mtawanyo kutoka moja hadi nne.

Pia, kuna ongezeko la kampuni za bima kutoka 32 mwaka 2021 hadi kampuni 35 huku wawekezaji wengi wakivutiwa na mazingira mazuri ya uwekezaji nchini.

Jambo lingine, Dkt.Baghayo Saqware amesema, Serikali imefanikiwa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 na kanuni zake.

“Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya 2023 inatoa nafasi kaa wananchi kupata huduma za afya kwa wingi na sahihi, na sheria hii inaenda kuongeza watumiaji wa huduma za afya, kuboresha maisha ya wananchi hasa watakapopata kadi za afya. Aidha, sheria hiyo inatoa nafasi NHIF kuwa chini ya uangalizi wa TIRA.”

Aidha, amesema Serikali imefanikiwa kufanya maboresho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2022. Serikali iliona ni muhimu kwa miradi yake inayotekelezwa nchini kuwa inakatiwa bima ili kuilinda pamoja na miundombinu.

Dkt.Saqware amesema, jambo lingine ni kuanzishwa kwa consortium ya kilimo ambayo ina kampuni 15 na consortium ya mafuta na gesi ambapo kuna umoja wa kampuni 22 ili kushiriki katika uchumi wa mafuta na gesi nchini kama sekta.

Katika hatua nyingine, amesema wamefanikiwa kuimarishwa kwa mifumo ya TEHAMA kutokana na maelekezo ya Rais Dkt.Samia ambapo mamlaka imepiga hatua kubwa na imeweza kuunganisha mfumo wake na Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, LATRA,TASAC na NIDA.

“Matarajio ni kuunganisha taasisi zaidi ya 30 bara na visiwani ili wananchi waweze kupata huduma kwa urahisi.”

Post a Comment

Previous Post Next Post

Contact Form