Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imethibitisha kuwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametengua
uteuzi wa Balozi Hamphrey Polepole, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini
Cuba, na kumwondolea rasmi hadhi ya ubalozi.
Taarifa hiyo
imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Balozi Dk. Samwel Shelukindo, kufuatia barua rasmi
iliyopokelewa kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses
Kusiluka.Kwa mujibu wa barua hiyo, Rais Samia, kwa kutumia
mamlaka aliyopewa chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma, amechukua hatua mbili kuu
dhidi ya Polepole Kutengua uteuzi wake kama Balozi wa Tanzania nchini
Cuba, Kumuachisha kazi rasmi kwa manufaa ya umma
Taarifa hiyo imeeleza kwamba, hatua hizo zimeanza kutekelezwa rasmi kuanzia tarehe 16 Julai 2025.
Hamphrey
Polepole, ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu serikalini
na ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikuwa amepelekwa kuiwakilisha
Tanzania nchini Cuba kama balozi, nafasi aliyoshika hadi uteuzi wake
ulipotenguliwa.
Wizara ya Mambo ya Nje imeeleza kuwa hatua
nyingine za kiutumishi na kidiplomasia kuhusu nafasi hiyo zitatolewa kwa
wakati muafaka, kadri taratibu za uteuzi mpya zitakavyokamilika.