Chama Kikuu
cha Ushirika Mkoa wa Iringa (IFCU) kimeendelea kutoa mafunzo kwa
wanachama wa vyama vya ushirika (AMCOS) yanayolenga kuanzisha huduma
ndogo za kifedha na kupunguza ukatili wa kijinsia.
Akizungumza
wakati wa semina hiyo Agost 5, 2025 Ukumbi wa Maktaba, Manispaa ya
Iringa, Mhasibu wa IFCU Mkoa wa Iringa Flora Mwaipungu amesema mafunzo
hayo ni muhimu ili wanachama waamke kiuchumi kwa kuanzisha SACCOS ndogo
au kuimarisha zile zilizopo na hivyo kuongeza kipato cha kaya zao. Amesema pia mafunzo yanasaidia kuhakikisha wanachama wanakuwa na usawa wa kijinsia katika AMCOS zao.
Naye
Afisa Maendeleo Manispaa ya Iringa Ester Sanga smesisitiza umuhimu wa
wanachama kuwa na huduma ndogo za kifedha wa kujiunga kwa pamoja ili
kukuza kipato cha kaya, kuanzisha biashara, kufanya kilimo cha kisasa na
kuondoa mikopo umiza yenye riba kubwa inayodai giza kwenye madeni na
kuwadidimiza kiuchumi.
Aidha amewataka wanachama kupeleka elimu kwa wengine na kuhakikisha hakuna ukatili wa kijinsia ili kutoa fursa sawa kwa wote.
Kwa
upande wao Wanachama walioshiriki wamekishukuru chama kikuu cha
ushirika Mkoa wa Iringa (IFCU) kwa mafunzo hayo kwani yametoa motisha
kwa wanaume na wanawake kushirikiana katika kuanzisha huduma ndogo za
kifedha na kutoa taarifa za ukatili katika maeneo yao huku akisisitiza
umuhimu wa kushirikiana kikamilifu katika kuboresha kipato na huduma za
kifedha za wanachama.