Waziri wa
Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, amewasili katika Wilaya ya Namtumbo,
Mkoa wa Ruvuma kwa ziara maalum ya kukagua maandalizi ya ziara ya
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan.
Ziara hiyo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatarajiwa
kufanyika tarehe 30 Julai 2025 ambapo atazindua Kiwanda cha Uchenjuaji
wa Madini ya Urani pamoja na kuzindua rasmi ujenzi wa Mgodi wa Urani
katika eneo hilo. Mradi huu mkubwa unatekelezwa na Kampuni ya Mantra
Tanzania Ltd, na unakadiriwa kugharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 3.06.
Katika
ukaguzi wake, Waziri Mavunde alieleza kuwa Serikali imejipanga
kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa kwa kuzingatia
masuala ya usalama wa mazingira, ajira kwa Watanzania, pamoja na
kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.
Aidha,
alisisitiza kuwa uwekezaji huo mkubwa ni ishara ya imani ya wawekezaji
kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu
Hassan, na kwamba mafanikio ya mradi huu yatafungua fursa nyingi kwa
wananchi wa Ruvuma na Watanzania kwa ujumla.
Kiwanda hicho na
mtambo mkubwa wa kuchenjua madini ya urani vinatarajiwa kuongeza thamani
ya madini hayo hapa nchini, kuimarisha mapato ya serikali, pamoja na
kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo la mradi.