Idadi ya Watia nia 208 wamejitokeza kuchukua fomu nafasi ya udiwani kwenye kata 29 za wilaya ya Morogoro Mjini ambapo nafasi ya ubunge ni wagombea 17 pekee. Akizungumza katika ofisi za CCM Wilaya ya Morogoro mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Morogoro Mjini Twalibu Kassimu Berege ametoa mchanganuo wa idadi ya wagombea nafasi ya udiwani katika kata zote.
Ameongeza kuwa “kutamatika kwa zoezi hilo kunatoa nafasi ya kuanza kwa vikao vya mchujo kwaajili ya kuwajadili wagombea na kutoa mapendekezo ambapo tarehe 4 wataanza ngazi ya kata na tarehe 6 ngazi ya wilaya na kuendelea kwahiyo tunawataka wanachama waliochukua fomu na kugombea waendelee kuwa watulivu waamini vikao ngazi ya kata,wilaya na ngazi ya mkoa kwa uteuzi nafasi ya madiwani na Taifa kwa ngazi ya Ubunge tunategemea kwamba chama kitawaletea watu wazuri watu watakokwenda kufanya ushindani kwenye soko la siasa la chama cha mapinduzi na wapinzani kwahiyo tunategemea watu tutakaowarudisha watauzika”.
Kwa upande wa Jumuiya za chama cha mapinduzi wamejitokeza wanachama kuchukua na kurejesha fomu ambapo Jumuiya ya Umoja Wa Vijana wa CCM mkoa wamejitokeza wanachama 5 kuchukua fomu na 4 kati yao wamefanikiwa kurejesha huku 1 akishindwa kurejesha fomu,Jumuiya ya Umoja wa wanawake Tanzania wamejitokeza wanachama 31 kuchukua na wote wamerejesha pamoja na Jumuiya ya Wazazi wamejitokeza wanachama 2 kuchukua na kufanikiwa kurejesha.