Mfuko wa
Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umetoa elimu ya hifadhi ya Jamii na
kueleza maboresho mbalimbali ya huduma zake, katika Mkutano Mkuu wa
Umoja wa Wanawake Wamiliki wa Shule na Vyuo vya Kati Tanzania (TAWOSCO),
uliofanyika tarehe 23 Julai, 2025 jijini Mwanza.
Akifungua
mkutano huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Profesa Adolf
Mkenda alieleza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na
TAWOSCO katika sekta ya elimu, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa
aliyoyafanya kwenye sekta ya elimu nchini.
Katika hafla hiyo,
Prof. Mkenda alikabidhi tuzo kwa waajiri wanaowasilisha michango ya
wafanyakazi wao kwa wakati katika Mfuko wa NSSF, ikiwa ni njia ya
kutambua na kuthamini uadilifu wao katika kutekeleza wajibu huo muhimu
wa kisheria na kijamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,
Mhe. Saidi Mtanda aliwapongeza wanawake wa TAWOSCO kwa mchango wao
kwenye maendeleo ya elimu, sambamba na kumshukuru Rais Dkt. Samia kwa
kuwekeza katika mkoa huo, hususan kuboresha miundombinu ya elimu na
huduma za kijamii.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa
NSSF, Bw. Masha Mshomba, Meneja wa Uandikishaji, Ukaguzi na Matekelezo
wa Mfuko huo, Bw. Cosmas Sasi alieleza kuwa hadi sasa, wanachama 131 wa
TAWOSCO sawa na asilimia 66 wamejiunga na NSSF, huku wanachama 35 kati
yao wakichangia michango ya wafanyakazi wao kwa ufanisi kila mwezi.
Aidha,
Bw. Sasi aliwasihi wanachama wenye malimbikizo ya michango kufika
katika ofisi za NSSF ili kuwasilisha mipango ya ulipaji wa madeni yao,
badala ya kusubiri hatua za kisheria ambazo zinaweza kuepukika kwa
kushirikiana kwa karibu na Mfuko.
Akizungumzia maboresho ya
huduma, Bw. Sasi alisema kuwa Mfuko umeanzisha mifumo ya kidijitali kama
vile NSSF Portal yaani Lango la Huduma linalojumuisha huduma binafsi ya
mwanachama, huduma binafsi ya mwajiri, NSSF App, WhatsApp Chatbot,
huduma za USSD na SMS, ambazo zinawezesha wanachama na waajiri kupata
huduma kwa urahisi zaidi bila kulazimika kufika ofisini.