Katika juhudi
za kuimarisha usafi wa mazingira na kuleta mabadiliko chanya katika
Jamii, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na Halmashauri
zake wamehitimisha ziara ya kimafunzo Mkoani Iringa ikiwa lengo ni
kujifunza kwa nadharia na Vitendo juu ya mifumo ya usimamizi wa usafi wa
mazingira, ushirikishwaji wa jamii, na mbinu za kuzuia magonjwa ya
mlipuko.
Ziara hiyo ambayo ilikuwa ni ya siku 4 imehitimishwa
July 22, 2025 katika Halmshauri ya Wilaya ya Iringa, Kijiji cha Ufyambe
Timu hiyo kutoka Mwanza ambayo imejumuisha Afisa Afya wa Mkoa, Katibu wa
Afya wa Mkoa, pamoja na Waganga Wakuu wa Halmashauri za Mkoa pamoja na
Maafisa Afya kutoka Halmashauri za Jiji la Mwanza, sengerema, misungwi
na llemela. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba
amesema ziara hiyo itakwenda kuleta tija ambapo kupitia uzoefu huo
walioupata utatumika kuleta maboresho ndani ya Mkoa wa Mwanza.
"Mkoa
wa Iringa umekuwa ni moja ya Mikoa ambayo inafanya vizuri katika zile
tatu bora Tanzania na sisi Mwanza mazingira yetu na Iringa yanafanana
tunataka na sisi kuboresha katika maeneo yetu ili kuzuia magonjwa ya
mlipuko" amesema Lebba
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa
Iringa Silvia Mamkwe amesema kutokana na Mkoa wa Iringa kufanya Vizuri
katika afua ya Mazingira imekuwa mfano wa kuigwa ambapo imehakikisha
imefikia kaya zaidi ya asilimia 98 zimefanikiwa kuwa na Vyoo lakini pia
kaya zaidi ya asilimia 95 kuwa na vyombo vya kunawia mikono.
Aidha
amesema kuwa Mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mkubwa wa
Wananchi pamoja na Uongozi wa Mkoa huku akitoa wito kwa Wakazi wa Iringa
kuhakikisha wanaendelea kutunza mazingira ili kuendelea kuwa kinara wa
usafi kitaifa.