MKUU wa mkoa wa Morogoro,Adam Malima amefanya ukaguzi wa zoezi la uchimbaji visima vya maji safi na salama ndani ya manispaa ya Morogoro eneo la kata ya Mafisa ikiwa ni sehemu ya maendeleo na kuhakikisha wananchi wa manispaa hii wanapatiwa mahitaji muhimu.
Serikali kwa
kushirikiana na Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Mamlaka ya Maji safi na
usafi wa Mazingira Morogoro(MORUWASA) na Wakala wa Maji na usafi wa
Mazingira vijijini (RUWASA) imeendelea kutatua changamoto ya upatikanaji
wa huduma ya maji kwa kuchimba visima kwenye maeneo mbalimbali ya
Manispaa ya Morogoro.
Juhudi hizo zimeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya Maji safi na salama kwa urahisi.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa uchimbaji wa mojawapo ya kisima kilichopo
Kayenzi, Kata ya Mafisa, chenye urefu wa mita 120, Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro, Adam Malima amesema kisima hicho kitapunguza kwa kiwango
kikubwa tatizo la maji kwani kitawanufaisha wakazi zaidi ya Laki moja.
Malima
ameendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda maeneo ya visima kwa
kuyatambua kama hifadhi za maji ambapo ameelekeza mamlaka husika
kuhakikisha wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya miradi hiyo wanalipwa
fidia stahiki na kuhamishiwa maeneo mengine ili kuruhusu utekelezaji wa
miradi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la
Wami/Ruvu, Elibariki Mmasy, ameeleza tayari wamebaini jumla ya maeneo 17
yenye vyanzo vya kuchimbwa visima ambapo 7 tayari vimechimbwa na
vimeonyesha matokeo chanya.
Naye, Meneja (RUWASA) Mkoa wa
Morogoro, Mhandisi Sospeter Lutonja, amesema kuwa hadi sasa jumla ya
visima 66 vimechimbwa katika mkoa huo.
Tags
Habari