Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ametoa wito kwa Shirika la Madini la
Taifa (STAMICO) kuwekeza kikamilifu katika rasilimali za madini
zinazopatikana katika Mkoa huo na kusisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia
kuongeza thamani ya madini, kutoa ajira kwa wananchi na kuchochea
maendeleo ya uchumi wa Mkoa na taifa kwa ujumla.
Senyamule ametoa
wito huo alipotembelea katika banda la STAMICO wakati wa Maonesho ya
Kilimo ya NaneNane yanayoendelea jijini Dodoma. Akizungumza baada
ya kukagua shughuli na bidhaa zinazotolewa na STAMICO, Senyamule
ameeleza kuwa Mkoa wa Dodoma umebarikiwa kuwa na aina mbalimbali za
madini, ikiwemo madini ya Gypsum, Chokaa, Manganese, Shaba pamoja na
madini ya ujenzi kama kokoto na mchanga na kusema kuwa uwekezaji wa
STAMICO unaweza kusaidia kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wakazi wa
Mkoa huo na kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa.
"STAMICO
ni taasisi ya serikali yenye uwezo mkubwa wa kitaalamu na kifedha, hivyo
naiomba itumie fursa hii kuwekeza zaidi hapa Dodoma. Tuna rasilimali
nyingi ambazo bado hazijachunguzwa wala kuendelezwa ipasavyo.
Ushirikiano wa karibu kati ya serikali ya Mkoa na STAMICO unaweza kuleta
mapinduzi katika sekta ya madini,” amesema Senyamule.
Kwa upande
wake, Afisa Uhusiano Mwandamizi a STAMICO Bibiana Ndumbaro amemweleza
Mkuu wa Mkoa kuwa Shirika hilo tayari limeanza Uchimbaji na uuzaji wa
kokoto jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa Shirika linaendelea kufanya
utafiti kwenye maeneo yake mbalimbali ya uwekezaji katika madini ya
kimkakati nchini, huku Dodoma ikiwa miongoni mwa maeneo yenye vipaumbele
kutokana na utajiri wa rasilimali madini zilizopo.
Maonesho ya
Nanenane ni jukwaa muhimu la kuonesha teknolojia na fursa mbalimbali
katika sekta za kilimo, ufugaji, viwanda na madini, na huwakutanisha
wadau kutoka sekta za umma na binafsi. Shirika la STAMICO ni miongoni
mwa taasisi zinazoshiriki kikamilifu katika maonesho hayo kwa lengo la
kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli zake na fursa zilizopo katika
sekta ya madini.