Mgombea
Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Ukonga, Ndugu
Alawi Abdallah Rwegoshora, ameibuka kuwa mmoja wa wagombea wenye
ushawishi mkubwa zaidi katika kinyang’anyiro cha kura za maoni, kufuatia
ahadi zake zenye mwelekeo wa maendeleo makubwa kwa wakazi wa jimbo
hilo.
Ndugu Alawi, ambaye pia ni Katibu wa Jumuiya ya Watanzania
waishio China, ameweka bayana dhamira yake ya kuliletea Ukonga
mabadiliko kupitia miradi yenye tija. Miongoni mwa ahadi kubwa
alizotoa ni upatikanaji wa mashine tatu za kuchimba barabara (Excavator
3) - yatakayotumika kuboresha miundombinu ya barabara ndani ya jimbo
hilo, hatua itakayopunguza changamoto za usafiri na kuimarisha huduma za
kijamii na kiuchumi.
Aidha, ameahidi kutoa fursa za elimu kwa
vijana watatu kila mwaka kwa kuwapeleka kusoma shahada nje ya nchi
kupitia ushirikiano wake na taasisi mbalimbali za kimataifa; hatua hiyo
inalenga kuongeza idadi ya vijana waliobobea kitaaluma na kurudi
kulijenga taifa.
Katika eneo la uchumi, Alawi ameweka mkazo
kwenye ujenzi wa soko jipya la kisasa katika eneo la Gongolamboto ambapo
mchakato wa awali wa utekelezaji umeshaanza kwa kushirikiana na wadau
wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi.
Mradi huo unalenga kuinua wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wa eneo hilo.
Kwa
mujibu wa Alawi, jitihada hizo ni za kibinafsina hazitegemei fedha za
Serikali au bajeti ya jimbo, jambo ambalo limeongeza imani ya wananchi
kwa mgombea huyo kutokana na moyo wake wa kizalendo na kujitolea.
Alawi
ametoa ahadi hizo katika majukwaa mbalimbali ya kampeni ya kuelekea
mchakato wa kura za maoni wa CCM unaotarajiwa kufanyika kesho, tarehe 04
Agosti 2025.
Sera zake zenye mvuto kwa jamii zimeibua ari mpya na hamasa kubwa miongoni mwa wajumbe wa chama na wananchi kwa ujumla.
Jimbo la Ukonga sasa limewaka moto huku jina la Alawi Abdallah likitajwa kama chaguo la wengi kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.