Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb)
amewasili jijini Minsk, Belarus kwa ziara ya kikazi ya siku nne kuanzia
tarehe 21 hadi 24 Julai 2025.
Alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege
wa nchi hiyo, Mhe. Waziri Mkuu alipokewa na Naibu Waziri Mkuu wa
Belarus, Mhe. Viktor Karankevich na viongozi wengine waandamizi wa nchi
zote mbili akiwemo Waziri wa Uwekezaji, Zanzibar, Mhe. Sharif Ali
Sharif; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Cosato Chumi na Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Mhe. Fredrick
Kibuta.
Ziara hiyo ambayo ni ya kwanza kwa Kiongozi wa ngazi ya
juu nchini Tanzania kuifanya nchini Belarus, inalenga kuendeleza mkakati
wa Serikali zote mbili wa kuimarisha uhusiano wa uwili hususan katika
sekta za kimkakati ikiwemo Kilimo, elimu, afya, utalii, uwekezaji,
biashara na uhaulishaji wa teknolojia.
Wakati wa ziara hiyo, Mhe.
Waziri Mkuu atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa
Belarus, Mhe. Alexander Turchin. Aidha, atatembelea na kufanya
mazungumzo na viongozi wa kampuni mbalimbali za nchini Belarus kwa lengo
la kuzishawishi kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Mheshimiwa
Waziri Mkuu pia atashuhudia uwekaji saini wa Hati za Makubaliano (MoUs)
kati ya Tanzania na Belarus zinazohusu kushirikiana katika maeneo
mbalimbali ikiwemo Mashauriano ya Kisiasa, kilimo, elimu na biashara.
Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Sera ya Mambo ya Nje inayolenga kukuza Doplomasia ya Uchumi.