Katibu wa
Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, amepongeza taasisi za Umma kwa
kupiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma
kwa umma kwani yameongeza ufanisi.
Mhandisi Zena ameyasema hayo
Julai 23, 2025 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Maafisa
Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala (TAPA-HR) katika ukumbi wa Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa, AICC jijini Arusha.Kauli mbiu ya
mkutano huo ni 'Mwelekeo mpya wa nafasi ya wataalamu wa usimamizi wa
rasilimali watu na utawala kusukuma mabadiliko kuendana na mageuzi ya
teknolojia'.
“Wakati natembelea mabanda ya Maonesho hapo nje,
nimeelezwa kila nilipoenda jinsi matumizi ya huduma mtandao
yalivyoongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi hili ni jambo
zuri.” Alisema.
Kabla ya kufungua mkutano huo, Mhandisi Zena
alitembelea mabanda ya Maonesho likiwemo banda la Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ambapo Afisa Uhusiano wa PSSSF, Bi.
Aisa Kimaro, alimueleza Mhandisi Zena kuwa kwa zaidi ya asilimia 95,
huduma za PSSSF zinatolewa kwa njia ya mtandao (PSSSF Kidijitali) hali
ambayo imeongeza ufanisi katika utoaji huduma.