Katika tukio
la kihistoria lililojawa na hisia za shukrani na heshima, taasisi isiyo
ya kiserikali ya Foundation for Disabilities Hope (FDH) imetunuku tuzo
maalumu kwa Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania
(TANAPA), CPA (T) Musa Nassoro Kuji, kwa niaba ya shirika hilo, ikiwa
ni kutambua mchango mkubwa wa TANAPA katika kuendeleza huduma jumuishi
kwa watu wenye ulemavu nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo
iliyofanyika leo, Julai 18, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa TANAPA
jijini Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa FDH, Bw. Maiko Salali, alieleza
kuwa TANAPA imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watu wenye
ulemavu wananufaika ipasavyo na vivutio vya utalii pamoja na huduma
jumuishi ndani ya Hifadhi za Taifa.
"Upendo wenu umeleta
mabadiliko chanya na umechipua mizizi ya mafanikio yaliyojengwa sanjari
na nia yenu njema kwa watu wenye ulemavu," alisema Bw. Salali.
Aidha,
aliongeza kuwa mchango wa TANAPA umechangia si tu katika ustawi wa
kijamii bali pia katika kuinua uchumi wa watu wenye ulemavu kupitia
fursa mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo.
"Tunatambua
na kuthamini sana juhudi zenu. TANAPA ni mfano wa kuigwa kwa kufanya
huduma zake kuwa jumuishi. Tunapokuja TANAPA, tunajisikia tuko nyumbani.
Maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusaidia watu wenye
ulemavu mnayaendeleza kwa vitendo," alisisitiza Bw. Salali.
Kwa
upande wake, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, CPA (T) Musa Nassoro Kuji,
alieleza kuwa dhamira ya shirika ni kuhakikisha mazingira ya hifadhi
yanakuwa rafiki kwa watu wote bila ubaguzi.
"Kuweka
mazingira rafiki na jumuishi kwa watu wote ndiyo dhamira kuu ya TANAPA,
na tutaendelea kufanya hivyo kwa mustakabali wa Taifa letu," alisema
Kamishna Kuji.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Naibu Kamishna wa
Uhifadhi, Massana Mwishawa, maafisa waandamizi wa TANAPA, askari wa
uhifadhi pamoja na wawakilishi waandamizi kutoka FDH.