Serikali
kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA),
imeandaa mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo Maafisa Maendeleo ya
jamii kutoka ngazi ya kata hadi mkoa, mkoani Iringa kwa lengo la
kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kunufaika na fursa ya
asilimia 30 ya zabuni za umma.
Akifungua mafunzo hayo Julai 11,
2025 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa M, Naibu Katibu Mkuu wa wizara
hiyo, Felista Mdemu, amesema serikali imedhamiria kuhakikisha makundi
maalum yanashiriki kikamilifu katika mifumo rasmi ya uchumi kwa kutumia
fursa ya asilimia 30 ya zabuni zilizotengwa kwa mujibu wa Sheria ya
Manunuzi ya Umma, Sura 410.
"Serikali imefungua milango, na sasa
tunahitaji kuona maafisa maendeleo ya jamii wakichukua nafasi ya kuwa
walimu na washauri wa vikundi ili viweze kujisajili, kujiandaa na
kushiriki katika zabuni hizo," amesema Mdemu.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Patrick Golwike, amefafanua kuwa
changamoto kuu kwa makundi maalum si ukosefu wa fursa, bali ni
maandalizi duni, ukosefu wa nidhamu ya kibiashara na kutokuelewa
taratibu za kushiriki zabuni.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara
ya Maendeleo ya Jamii, Juliana Kibonde, alisema kuwa mafunzo hayo ni
sehemu ya mkakati mpana wa kuwajengea uwezo maafisa maendeleo ya jamii
ili waweze kuhamasisha uundwaji wa vikundi vipya na kuviunganisha na
mifumo rasmi ya manunuzi na uchumi.'
Katibu Tawala Msaidizi wa
Mkoa wa Iringa, Venance Ntyarundula, amesema kuwa mkoa umejipanga
kuandaa kongamano la kila mwaka la maafisa maendeleo ya jamii, ili
kutathmini utekelezaji wa sera na programu zinazolenga kuboresha maisha
ya makundi maalum.
"Tunaanza mwaka huu wa fedha kwa mtazamo
mpya. Tunataka kuona vikundi vikipewa zabuni, wakipata mapato, na
hatimaye kubadilisha maisha yao. Hii ni njia ya kuhakikisha hakuna
mwananchi anayebaki nyuma katika maendeleo ya taifa," amesema
Ntyarundula.