Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Agosti 13, 2025 kutoa uamuzi juu ya hoja
zilizoibuliwa baina ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu na Upande wa
Serikali katika kesi ya uhaini.
Kesi ya Lissu ilitajwa leo mbele
ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franko Kiswaga ambapo Jopo la Mawakili wa
Upande Jamhuri uliongozwa na Nassoro Katuga, huku Lissu akijitetea
mwenyewe.
Mbali na hoja nyingine, Lissu aliiomba mahakama hiyo
kutupilia mbali kesi hiyo ikiwezekana kuifuta kutokana na Upande wa
Jamhuri kuichelewesha licha ya upelelezi kukamilika.
“Kwa mara ya
kwanza naomba uwaambie mahakama hii isiahirishe kesi, huu mchezo ni
ukatili sana, nipo mahabusu ninaishi na wafungwa waliohukumiwa kifo ili
nianze kuzoea zoea, wakatilie mheshimiwa ama kesi ifutwe,”.
Kwa
upande wake wakili Katuga aliiomba mahakama hiyo iahirishe kesi kwa kuwa
wanasubiri uamuzi wa Agosti 4, 2025 katika Mahakama Kuu ya Tanzania juu
ya hatma ya maombi yao ya kuwalinda mashahidi kama yatakubaliwa ama la.
“Mahakama
Kuu imepanva kutoa uamuzi ambao tunausubiri ili tuwasilishe taarifa
kwani mahakama yako haiwezi kutoa amri kwa Mahakama Kuu hivyo hatuna
budi kusubiri maamuzi hayo,”.
Kutokana na mvutano huo uliochukua takribani saa moja na nusu, Hakimu Kiswaga alisema;
“Leo
hii sitatoa maamuzi madogo nitaahirisha na sababu ni kwamba imekuwa
kawaida natiaga maamuzi hapa hapa ila mawasilisho ya leo yamekuwa ni
yale ambayo yanawasilishwaga hapa na hata kesi zilizotumika pia, hivyo
mahakama inahitaji muda. Naahirisha kesi hadi tarehe 13, 8, 2025,”.
Katika
kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini akidaiwa kutenda
kosa hilo April 3, 2025 kwa madai ya kuhamasisha kuzuia Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2025.