Marekani imethibitisha kuwa imefanya mashambulizi ya anga dhidi ya vituo vitatu vya nyuklia nchini Iran.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema mashambulizi hayo yamefanyika kwa mafanikio na kwa ushirikiano na Israel.Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu ya Marekani, mashambulizi hayo yalilenga kuzuia maendeleo ya programu ya nyuklia ya Iran, ambayo imekuwa ikionekana kama tishio kwa usalama wa kimataifa.
Vituo vilivyolengwa vinadaiwa kuwa sehemu ya uzalishaji na usafishaji wa madini ya uranium.
Mashambulizi haya yamekuja siku chache tu baada ya Israel kufanya operesheni kadhaa za kijeshi dhidi ya Iran, ambapo Marekani ilikuwa imeonya kuwa ingejiunga iwapo Iran haitasitisha urutubishaji wa uranium ndani ya kipindi cha wiki mbili.
Wakati marekeni ikijiunga kwenye vita hiyo, Serikali ya Iran, kupitia msemaji wake wa wizara ya mambo ya nje, imelaani vikali mashambulizi hayo na kuonya kuwa kitendo hicho ni tangazo la wazi la vita.
Iran imetishia kulipiza kisasi kwa kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani na washirika wake Mashariki ya Kati.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa hali ya tahadhari imetangazwa katika maeneo ya kijeshi ya Marekani yaliyoko katika nchi za Ghuba, huku mataifa ya Kiarabu yakitoa wito wa kuzuia kuongezeka kwa mzozo huo.