Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein
Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kutekeleza
miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar kwa lengo la
kuboresha maisha ya wananchi.
Rais
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 02 Januari 2026, alipokuwa
akizungumza na waumini wa Dini ya Kiislamu wa Msikiti wa Ijumaa wa
Unguja Ukuu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja baada ya kuungana nao
katika ibada ya Sala ya Ijumaa.
Amesema
ujenzi wa Daraja la Uzi Ng’ambwa pamoja na barabara zake, ambao kwa
muda mrefu umekuwa kilio cha wananchi, umefikia hatua nzuri na
unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi minne ijayo. Rais Dkt.
Mwinyi ameielezea hatua hiyo kuwa ni mafanikio makubwa kwa wananchi wa
eneo hilo na Zanzibar kwa ujumla.
Aidha,
amesema Serikali inaendelea kujipanga kutafuta ufumbuzi wa changamoto
nyingine zinazowakabili wananchi, ikiwemo miundombinu ya barabara na
upatikanaji wa maji safi na salama. Katika hatua hiyo, ameeleza kuwa
Serikali itawatuma wataalamu wake katika siku za karibuni ili kufanya
tathmini na kubaini njia bora za kutoa ufumbuzi wa kudumu wa changamoto
hizo.
Rais Dkt. Mwinyi
amewanasihi wananchi kuendelea kudumisha amani na kuiombea nchi,
akisisitiza kuwa amani ni nguzo muhimu ya maendeleo. Amesema kuwa kuwepo
kwa amani kunawezesha Serikali kukusanya mapato kwa ufanisi na
kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kiwango kikubwa zaidi.
Kwa
muda mrefu sasa, Rais Dkt. Mwinyi ameendelea kuimarisha utaratibu wa
kuungana na waumini wa Dini ya Kiislamu katika ibada ya Sala ya Ijumaa
kwenye misikiti mbalimbali, mijini na vijijini.





0 Comments