VITA ya nani mchezaji bora wa ligi kuu ya NBC(MVP) wa msimu wa 2024-25 ipo mbioni kukamilika na punde TFF imesema mwezi ujao itamtangaza hadharani MVP huyo kati ya Pacôme wa Yanga au Ahoua wa Simba SC.
Jean Charles Ahoua, nyota wa zamani wa Stella Club d’Adjame, alikuwa MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliopita 2023-2024.
Pacome Zouzoua ambaye pia alimaliza msimu wa 2022-2023 kwa kuibuka MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast.
Wakali hao wanaocheza eneo la kiungo cha ushambuliaji, wote ni raia wa Ivory Coast na wanatajwa kuchuana vikali katika tuzo hiyo, hapa kuna mchango wa kila mmoja kuanzia kufunga, kutengeneza mabao na tuzo za mchezaji bora wa mechi.
MCHEZAJI BORA WA MECHI
Katika kila mchezo wa Ligi Kuu Bara ulipomalizika, amekuwa akichaguliwa mchezaji bora na Pacome amefanikiwa kuchaguliwa mara nane.
Kiungo huyo ndiye anaongoza kutwaa tuzo nyingi zaidi za mchezaji bora wa mchezo msimu huu akifuatiwa na Jean Charles Ahoua ambaye amechukua mara tano huku Yanga pia ikiwa kinara wa nyota wake kuchukua mara nyingi zaidi ikichukua mara 24 kati ya 30, Simba ikishika namba mbili kwa kuchukua mara 21 kati ya 30.
MCHEZAJI BORA WA MWEZI
Hapa Ahoua amechukua tuzo moja ya mchezaji bora wa mwezi na alifanya hivyo Agosti 2024, ikiwa ni mwanzo wa msimu huu.
Kwa upande wa Pacome, hajabeba tuzo hiyo ambayo mchezaji aliyechukua mara nyingi ni Steven Mukwala wa Simba akibeba mara mbili.
Orodha ya waliobeba tuzo hiyo kila mwezi ipo hivi; kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua (Agosti 2024), aliyekuwa mshambuliaji wa Fountain, Gate Seleman Mwalimu (Septemba 2024), kiungo wa Singida Black Stars, Marouf Tchakei (Oktoba 2024), kiungo wa Tabora United, Offen Chikola (Novemba 2024), mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize (Desemba 2024), mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube (Februari 2025), mshambuliaji wa Simba, Steven Mukwala (Machi 2025), kiungo wa Dodoma Jiji, Iddi Kipagwile (Aprili 2025) na mshambuliaji wa Simba, Steven Mukwala (Mei 2025).
TAJI LA LIGI
Pacome alijiunga na Yanga msimu wa 2023-2024 akitokea Ligi Kuu ya Ivory Coast alikokuwa mchezaji bora wa msimu (MVP) na alikuja kuongeza nguvu katika eneo la kiungo mshambuliaji akisaidiana na Stephane Aziz Ki, kinara wa upachikaji mabao msimu huo akifunga 21 ambaye ametimka hivi karibuni kwenda Wydad Casablanca ya Moroco.
Ahoua ameipambania Simba kusaka taji la ligi lakini imeshindikana, huku Pacome akihusika moja kwa moja kwenye mchezo wa uamuzi akifunga moja na asisti moja wakati Yanga ikishinda 2-0 dhidi ya Simba.
MCHANGO WA MABAO
Msimu huu, Ahoua ameibuka kinara wa mabao, kwa jumla amehusika kwenye mabao 25, akifunga 16 na asisti tisa. Pacome amefunga mabao 12 na asisti 10, hivyo amehusika kwenye mabao 22.
Huu ukiwa ni msimu wa kwanza kwa Ahoua, namba zake zimekuwa juu kulinganisha na ilivyokuwa kwa Pacome wakati anatua Yanga 2023-2024 na alipachika mabao saba na asisti nne akihusika kwenye mabao 11.


