"MISA SI TAARABU" UJUMBE WA CARDINAL ARINZE KAMA KIOO CHA KUJITAZAMA KWA MAASKOFU WA TANZANIA

TAFAKURI YA LEO

Na. GODWIN CHARLES, Muumini Kanisa Katoliki

Ukisikiliza mahubiri ya baadhi ya maaskofu wa kanisa langu Katoliki kwa siku za hivi karibuni unaweza ukahisi ni nyimbo za mafumbo anaimbiwa mtu anayetakiwa kuupokea ujumbe maalum ambaye mwimbaji ana shida naye binafsi.

Unapomsikia Baba Askofu kama Kyando anasema “MACHAWA HAWAWEZI KUTUGAWANYA” unapata mashaka kuona ni kwa namna gani CHAWA anaweza kutumika kuligawa kanisa lenye sheria zake, miongozo na utaratibu maalum na ni Kwanini Baba Askofu apate hofu ya mambo yanayofikirika namna hii!

Ukirejea kinachoendelea sasa na namna waumini kadhaa walivyoamua kupaza sauti zao na lugha walizokutana nao kuwajibu kuanzia kwa Baba yangu Askofu Ruwaich na wenzake, utagundua kuwa Maaskofu hawa wamechagua kutumia njia kali kukabiliana na masuala mepesi yanayotaka tu kanisa na viongozi kusimama katika mstari wake dhidi ya malalamiko ya Padri Charles Kitima kuwa ni MSHAURI MWANDAMIZI WA CHADEMA.

Hapo ndio yanapoingia maono ya *Cardinal Francis Arinze,* mzaliwa wa Nigeria na aliyewahi kuwa Mkuu wa Idara ya Ibada ya Kimungu na Sakramenti Vatican, anabaki kuwa rejea ya juu katika kulinda heshima na utakatifu wa Misa Takatifu. 

Mafundisho yake yako wazi kuwa Misa ipo kwa ajili ya kumuabudu Mungu, kumshukuru, kuomba msamaha wa dhambi na kuomba msaada wa Mungu. 

Kwenye Miss hakuna nafasi ya burudani, vijembe, dharau au maonyesho ya hisia.

Tafakuri ya leo inatupeleka kujiangalia kwa kina, hasa pale tunapoona mwelekeo unaojitokeza katika baadhi ya madhabahu nchini Tanzania, ambapo Misa inaanza kuhama kutoka ibada kwenda maonesho, na maneno ya kejeli dhidi ya waumini yanapata nafasi. 

Hili ndilo onyo la Arinze linaloonya kuwa “ibada inapogeuzwa kuwa kitu cha kupimwa kwa makofi na vicheko, inakoma kuwa ibada”.

*Biblia inasema “Madhabahu si Mahali pa Dharau”

Maandiko Matakatifu yako wazi kuhusu lugha na mwenendo unaostahili mbele ya Mungu:

Mathayo 5:22: “Kila amkasirikiaye ndugu yake atapatikana na hatia…”* — dharau na matusi havina nafasi mbele ya madhabahu.

Na

*Yakobo 3:9–10: “Kwa ulimi huo tunamhimidi Bwana… na kwa huo huo tunawalaani wanadamu… Haifai iwe hivyo.”*

Na

*Mithali 15:1: “Jibu la upole hugeuza hasira, bali neno kali huchochea ghadhabu.”*

Na 

*Mathayo 7:3–5: Yesu anawakumbusha viongozi kujitathmini kwanza kabla ya kuwakosoa wengine.

Kwa msingi huu wa Kibiblia, madhabahu inapogeuzwa kuwa jukwaa la kejeli dhidi ya waumini, si waumini wanaopotoka bali ni ibada yenyewe inayopoteza mwelekeo.

UJUMBE KWA MAASKOFU WA TANZANIA 

Katika muktadha huu, kauli na mahubiri ya baadhi ya Maaskofu hususan Askofu Kyando, Askofu Ruwa’ichi na wengieo yamezua tafakuri nzito ya kiimani. 

Pale waumini wanapogeuzwa mada ya mipasho, na hoja zao kujibiwa kwa dharau, mipaka ya uchungaji hupitwa inatafakarisha sana

Tafakuri ya leo inakumbusha kuwa kukosoa si uasi, ni sehemu ya maisha ya Kanisa linalotambua kuwa viongozi ni wanadamu, nao wanahitaji uwajibikaji, unyenyekevu na kujitathmini.

VIONGOZI WENGINE WA DINI WALIOKEMEA CHUKI

Historia ya dini mbalimbali ina mifano ya viongozi waliokemea wazi matumizi ya madhabahu au mimbari kueneza chuki na dharau. Nitatoa mifano michache 

Pope (Papa) Francis amesisitiza mara kwa mara kuwa madhabahu *“si jukwaa la kushambulia wengine, bali mahali pa kuponya na kuunganisha.”*

Ameonya dhidi ya mahubiri yanayojengwa juu ya hasira na mgawanyiko badala ya Injili ya huruma.

Aidha, 

•Desmond Tutu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Afrika Kusini, aliwakemea hadharani viongozi wa kidini waliotumia Biblia kuhalalisha ubaguzi na chuki, akisema “Ukikitumia kitabu kitakatifu kudhalilisha wengine, umekipoteza kiini chake.”

Kadharika, 

Katika Uislamu, wanazuoni wengi wamekemea vikali khutba za misikitini zinazoeneza kejeli na chuki, wakirejea Qur’an (49:11): *“Wala msidharau watu wengine…”msimamo unaoonyesha kuwa heshima ya mahali patakatifu ni kanuni ya pamoja ya imani.

Mifano hii inaonyesha ukweli mmoja mkubwa kuwa dini yoyote inapohalalisha dharau mbele ya madhabahu, hupoteza sauti yake ya kimaadili.

SIASA NA MADHABAU - ONYO LA ARINZE

Ndani ya tafakuri hii, malalamiko dhidi ya Padri Dkt. Charles Kitima, yanayohusisha madai ya kulihusisha Kanisa na siasa za upinzani hasa CHADEMA yanapaswa kushughulikiwa kwa hekima

Cardinal Arinze anakazia kuwa Misa si mahali pa ajenda za kisiasa, hoja zikijibiwa kwa vijembe vya madhabauni, Kanisa linahatarisha umoja wake na kuonekana kama mshiriki wa mapambano ya kisiasa badala ya mama wa waumini wote.

Wapendwa, 

Tafakuri ya leo inatualika kurudi kwenye msingi wa imani:

Madhabahu si jukwaa la taarabu.

wala Misa si mahali pa dharau na kejeli Na 

kiongozi wa kiroho si mshereheshaji bali mchungaji.

Na 

Misa ni ya Mungu, si ya hisia zetu kwani Neno la Mungu linaitwa kuponya, si kuumiza.

Kama alivyoonya Cardinal Francis Arinze, ibada ikipoteza unyenyekevu wake, Kanisa litapoteza mamlaka yake ya kiroho. Tafakuri hii iwe mwaliko wa toba, kujitathmini na kurejea katika ibada yenye heshima, upendo na ukweli.

Post a Comment

0 Comments