RAIS SAMIA AAGIZA VIJANA WALIOFUATA MKUMBO OKTOBA 29 WAACHIWE

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuchuja kwa makini mashtaka ya vijana walioshtakiwa kwa kosa la uhaini kufuatia maandamano ya Oktoba 29, 2025.

Akihutubia Bunge leo tarehe 14 Novemba 2025, Rais Samia alisema kuna kundi kubwa la vijana waliokamatwa bila kuelewa uzito wa kile walichokifanya, huku wengine wakijihusisha katika maandamano kwa kufuata mkumbo bila dhamira ya kufanya uhalifu.

“Natambua kuna vijana wengi wamekamatwa kwa kushtakiwa kwa makosa ya uhaini—hawakujua wanachokifanya na wengine wamefuata mkumbo. Nikiwa kama Mama, navielekeza vyombo vya kisheria kuangalia makosa yaliyofanywa na vijana wetu. Kwa wale ambao walifanya mambo kwa kufuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu, wawafutie makosa yao.”

Akiendelea, alieleza kuwa rekodi na video za tukio la maandamano zinaonyesha wazi kuwa baadhi ya vijana walishiriki kwa ushabiki bila kuwa na nia ya kuvuruga amani. Kwa msingi huo, alitoa maagizo mahsusi kwa Ofisi ya DPP:

“Naelekeza Ofisi ya DPP kuchuja viwango vya makosa, na kwa waliofuata mkumbo wawaachie waende kwa wazazi wao.”

Post a Comment

Previous Post Next Post

Contact Form