Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali
Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji
wa miundombinu ya michezo kwa lengo la kuifanya Zanzibar kuwa kituo
maalum cha utalii wa michezo kitaifa na kimataifa.
Rais Dkt.
Mwinyi ameyasema hayo , aliposhiriki Bonanza la 16 la Mazoezi ya Viungo
lililoandaliwa na Chama cha Mazoezi ya Viungo Zanzibar (ZABESA),
lililofanyika katika Uwanja wa New Amaan Complex, Mkoa wa Mjini
Magharibi. Bonanza hilo limehusisha vikundi 165 vya mazoezi kutoka
vilabu 25 vya Pemba, 100 vya Unguja na 40 kutoka Tanzania Bara, likiwa
na washiriki zaidi ya 500.
Amesema mazoezi ya viungo ni nguzo
muhimu ya afya ya mwili na akili, na husaidia kuongeza kinga dhidi ya
magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la damu na magonjwa
ya moyo.
Aidha, amebainisha kuwa bonanza la kila mwaka ni jukwaa
muhimu la kuwakumbusha wananchi umuhimu wa afya njema kwa maendeleo ya
mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Rais Dkt. Mwinyi
amewahimiza wananchi kuendelea kushiriki michezo mbalimbali ikiwemo
mpira wa miguu, volleyball, riadha pamoja na michezo ya asili ya
kitamaduni ili kuimarisha afya zao. Ameeleza pia kuwa Serikali
itaendelea kuhimiza mabonanza, matukio ya michezo, ligi na mashindano ya
kitaifa na kimataifa ili kuongeza mvuto wa utalii wa michezo Zanzibar.
Amefafanua
kuwa michezo ni sekta muhimu inayochangia maendeleo ya utalii na uchumi
wa Taifa kwa kuvutia watalii na wawekezaji, kuongeza fursa za ajira kwa
vijana na kukuza pato la Taifa. Serikali, kwa kushirikiana na wadau wa
michezo, itaendelea kuimarisha miundombinu ili kufikia viwango vya
kitaifa na kimataifa na kuendeleza vipaji kuanzia ngazi ya chini hadi ya
juu.
Rais Dkt. Mwinyi amesema kupitia programu madhubuti za
mafunzo, nidhamu na usimamizi bora, Zanzibar inaweza kuzalisha
wanamichezo bora watakaoshindana kimataifa na kuinua hadhi ya Taifa
pamoja na kuboresha maisha yao na familia zao. Ameongeza kuwa Serikali
imeimarisha kwa kiwango kikubwa miundombinu ya michezo ikiwemo Uwanja wa
Amaan Complex, Gombani na Mao Tse Tung, sambamba na ujenzi wa viwanja
17 unaoendelea katika mikoa yote, ambapo baadhi tayari vimekamilika.
Mapema,
Rais Dkt. Mwinyi aliwaongoza mamia ya wana mazoezi katika matembezi
maalum kutoka Michenzani kupitia Muembe Kisonge hadi Uwanja wa New Amaan
Complex, kabla ya kushiriki mazoezi ya pamoja. Amewapongeza ZABESA na
wadau wote kwa kufanikisha bonanza hilo na kuwakabidhi vyeti vya
shukrani, huku akihimiza kuendelea kuliunga mkono. Aidha, alipata fursa
ya kusalimiana na mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania, mshindi wa
medali ya dhahabu ya mbio za marathon, Alphonce Simbu, aliyeshiriki
bonanza hilo.

0 Comments