WALIOPISHA UJENZI WA UWANJA WA AFCON ARUSHA WALIPWA BIL.2.3
Jumla ya Shilingi Bilioni 2.3 zalipwa kwa wananchi
Rc Makalla amshukuru Rais Samia kwa kuidhinisha fedha hizo za fidia
Aagiza malipo yafanywe haraka pasipo kuchelewesha
Serikali ya awamu ya sita imelipa Jumla ya Shilingi 2,386,970, 000 ikiwa ni fidia kwa wananchi wa Kata ya Olmot Wilayani Arusha, waliopisha ujenzi wa mradi wa uwanja wa Mpira wa Miguu utakaotumika kwaajili ya Michuano ya mpira wa miguu kwa Mataifa ya Afrika maarufu kama AFCON 2027.
Katika hafla hiyo iliyofanyika leo Disemba 31, 2025 ndani ya eneo kunakotekelezwa mradi huo wa ujenzi, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla mara baada ya kukabidhi hundi kwa wananchi waliopisha mradi huo, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha utoaji wa fedha hizo, akisema mradi huo unaenda kuupa Mkoa heshima na kusisimua uchumi wa Arusha.
"Nimekuja hapa kuruhusu utoaji wa fidia shilingi 2,386,970,000 ambazo Rais Samia ameziidhinisha na suala si pesa, suala ni ile dhamira ya kupisha kwaajili ya kitu cha maendeleo. Ninyi nyote mliopisha na kupewa fidia leo mnabaki katika kumbukumbu kwamba ni Watanzania wazalendo mnaopenda nchi yenu na kupisha maendeleo makubwa kama haya." Amesema Mhe. Makalla.
Akisisitiza kuwa fedha zipo na ni muhimu kulipwa kwa haraka kwa kila mwananchi anayestahili fidia hiyo, Mhe. Makalla pia amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano pale serikali itakapohitaji baadhi ya maeneo yao ikiwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara za njia nne kwa kiwango cha lami za kuingia katika uwanja huo.
Kulingana na Serikali, Jumla ya wananchi 12 watalipwa fidia katika fedha hizo, saba wakilipwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha na wengine watano watakaolipwa na Wizara ambapo eneo jumla lililotwaliwa na serikali linafanya jumla ya ekari 83 zilizotumika katika ujenzi wa uwanja huo wa michezo.
0 Comments