Na Ally Mandai
Anaandika Mbunge wa Jimbo la Mtumba na Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde.
Mwezi
September 2025 nikiwa katika Mtaa wa Sogeambele,Kata ya Chihanga-Dodoma
kwenye Kampeni ya Mtaa kwa Mtaa nikakutana na Mama mmoja ambaye aliomba
kuniuliza swali lakini baada ya kupewa 𝙈𝙖𝙞𝙠𝙞 hakuuliza swali na
badala yake aliangua kilio kikali akiniomba nimsaidie mwanaye Juma
Maganga aliye gerezani Juba,Sudan Kusini arejee uraiani na kuja kuungana
na familia yake.
Juma ni
dereva wa magari makubwa ambaye akiwa Sudan Kusini Tarehe 14.02.2025
alipata ajali ya kumgonga Mwanajeshi mmoja ambaye alipoteza maisha yake
na hivyo kupelekewa Juma kushikiliwa na vyombo vya sheria Sudan na
kuhitajika kulipa faini ya ng’ombe 51 sawa na Tsh 36,000,000 kwa mila na
desturi ya Sudan inapotokea ajali inayosababisha kifo kwa kuwa marehemu
alikuwa ameacha wake watatu na hivyo lazima wote wafikiwe na mgao
pamoja na wazazi wake.
Taratibu
za kuchangishana ziliendelea na kupitia watanzania waliopo Juba na
hapa nchini tulijitahidi kumchangia kumaliza changamoto hiyo lakini
fedha hiyo haikufika lengo na kumfanya Juma aendelee kusota gerezani kwa
miezi 10 huku akiwa amefungwa minyororo muda wote.
Sikujua
kama yule ni mama mzazi wa Juma lakini nikamjulisha Mama kwamba
nalifahamu tatizo la mwanaye na tunaendelea kumsaidia,nikampa taarifa tu
kwamba kwa muda wote akiwa gerezani;
-Namsaidia Chakula chake kule Sudan
-Naisaidia Familia yake iliyopo hapa Dodoma kupata mahitaji muhimu.
Nikamtia
moyo Mama kwamba Juma atatoka tumepata ushirikiano mkubwa wa serikali
kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na wakati Juma aliniambia inahitajika
Dola 2000 ili aachiwe huru fedha ambayo niliituma Mahakamani Sudan
kumsaidia kutoka lakini kwa bahati mbaya fedha ile haikusaidia kumtoa
Juma na aliendelea kushikiliwa.
Wiki
iliyopita Mtanzania mmoja aitwaye Nickson alinipigia simu na
kunijulisha kwamba wamejiridhisha kwamba ikipatikana Dola 1500 ziada ya
ile ya awali Juma ataachiliwa.
Tulifanya malipo ya Dola 1500 kule Mahakama ya Juba,Sudan tarehe 29.12.2025.
Jana Tarehe 31.12.2025 Juma ameachiliwa na sasa yupo njiani kurejea Nyumbani Dodoma,Tanzania.
Natumai Mama na Mke wa Juma siku ya leo itakuwa siku kubwa ya kumshukuru Mungu kwa matendo makuu aliyowatendea.

.jpg)


0 Comments