Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita @mboni_mhita amewatembelea wananchi waliokumbwa na athari iliyotokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali uliotokea usiku wa kuamkia Disemba 12, 2025, katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Msalala kwa lengo la kutoa faraja kwa wananchi hao
Akiwa katika ziara hiyo, RC Mhita ameagiza wananchi wote waliopata majeraha kutokana na kuangukiwa na nyumba waweze kupatiwa matibabu bure, huku jitihada za kurudisha makazi yao yaliyoathirika zikiendelea.
RC Mhita ameelekeza kusitishwa kwa huduma za uzazi katika Zahanati ya Mwanase kwa sababu za kiusalama lakini pia ametaka ukarabati wa haraka wa zahanati hiyo uanze mara moja ili huduma ziweze kurejea kwa wakati .
“Lengo letu ni kuhakikisha huduma za Afya hazikwami, lakini pia tunalinda usalama wa wananchi, eneo ambalo limeshathibitika kuwa na changamoto za kimazingira linapaswa kutumika kwa tahadhali kubwa.” Amesema RC Mhita.
Vilevile, RC Mhita amemuagiza Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kuhakikisha anapitia na kukagua miradi yote inayojengwa kwa nguvu za wananchi, kabla ya kuanza kutumika ili kuhakikisha yanajengwa katika ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Ndg. Abdulkadir Mfilinge, amesema kuwa hatua za awali zilizochukuliwa ni pamoja na kuhamishia huduma za afya kwa muda katika zahanati iliyo jirani na eneo lililoathirika, ili wananchi waendelee kupata huduma kwa wakati.

.jpeg)




0 Comments