RAIS MWINYI AFUNGUA NYUMBA ZA WAFANYAKAZI HOSPITALI YA KITOGANI, AAGIZA ZHC KUSIMAMIA UJENZI WA MAKAAZI YA WATUMISHI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema lengo la Serikali ni kuimarisha na kuongeza ubora wa huduma za afya kwa wananchi katika maeneo yote ya Zanzibar, sambamba na kuwapunguzia wafanyakazi wa sekta ya afya masafa ya kusafiri kwa kuhakikisha wanakuwa karibu na jamii wanayoihudumia.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 31 Disemba 2025 alipofungua nyumba za makaazi ya wafanyakazi wa Hospitali ya Kitogani, Mkoa wa Kusini Unguja.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameagiza miradi yote ya ujenzi wa nyumba za makaazi ya wafanyakazi wa Serikali isimamiwe na Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC), ili kuongeza ufanisi, kasi ya utekelezaji na kupunguza gharama za ujenzi. Ameielekeza Wizara ya Afya kujikita zaidi katika ujenzi wa hospitali na utoaji wa huduma za afya, badala ya kujenga nyumba za wafanyakazi, jukumu ambalo amesema ni mahsusi kwa Shirika la Nyumba la Zanzibar.

Ameeleza kuwa ZHC lina dhamana na uwezo wa kitaalamu wa kushughulikia masuala ya makaazi, kusimamia miradi ya ujenzi kwa ufanisi na kuhakikisha inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.

Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa baada ya Serikali kufanikisha ujenzi wa vituo vya afya na hospitali za wilaya katika wilaya zote 11 za Zanzibar, sasa inaelekeza nguvu katika kukamilisha ujenzi wa hospitali za mikoa katika mikoa yote mitano.

Vilevile, amefahamisha kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa hospitali tatu kubwa za rufaa, ambazo ni ujenzi mpya wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Hospitali ya Matibabu ya Saratani ya Binguni, pamoja na Hospitali ya Kujifunzia (Teaching Hospital) itakayojengwa Binguni. Amesisitiza kuwa hospitali hizo zote zitaambatana na nyumba za makaazi ya wafanyakazi.

Akizungumzia nyumba za makaazi za Kitogani alizozifungua, Rais Dkt. Mwinyi amesema ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kuwapatia wafanyakazi wa hospitali, hususan wataalamu wabobezi, makaazi bora yaliyo karibu na maeneo yao ya kazi. Amesema hatua hiyo itahamasisha watumishi, kuboresha utoaji wa huduma za afya, na kupunguza upungufu wa nyumba za makazi.









Post a Comment

0 Comments