Dar es Salaam.
Upinzani wa waumini wa Kanisa Katoliki dhidi ya mwenendo wa baadhi ya viongozi wa juu wa kanisa, akiwemo Padri Dkt. Charles Kitima na Askofu Mkuu Ruwa’ichi, unaendelea kushika kasi, huku hoja za kimaadili, kisheria na kiteolojia zikiwekwa wazi hadharani.
Kupitia tafakuri nzito ya dhamiri iliyotolewa na Mwalimu Ludovick Joseph, muumini wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania, waumini wameanza kujenga hoja ya pamoja kwamba Kanisa si mtu mmoja, si padri wala askofu, bali ni jumuiya ya waumini, na kwamba viongozi wa kanisa hawako juu ya Injili wala juu ya waumini.
Katika tafakuri hiyo, waumini wanasema wazi kuwa kuhoji, kukosoa na kuomba uchunguzi dhidi ya kiongozi wa kanisa si uasi, si dhambi wala si chuki, bali ni haki ya kisheria inayotambuliwa ndani ya mfumo wa Kanisa Katoliki lenyewe.
“Kanisa ni takatifu kwa sababu ya Kristo, lakini viongozi wake ni wanadamu wenye mipaka na wanaweza kukosea,” inaeleza tafakuri hiyo, ikisisitiza kuwa hakuna kiongozi aliye juu ya Injili.
MATUSI, KEJELI NA LUGHA YA DHARAU VYAKEMEWA
Waumini wameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu matumizi ya lugha ya dharau na kejeli dhidi ya waumini kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kanisa, wakisisitiza kuwa madhabahu si mahali pa matusi wala fedheha, bali ni eneo la kufundisha, kuponya na kuijenga jamii ya waamini.
Kwa kunukuu maandiko ya Biblia, tafakuri hiyo inabainisha kuwa lugha ya dharau haina nafasi katika mafundisho ya Kikristo na kwamba kiongozi wa kiroho anapaswa kuhubiri kwa unyenyekevu na neema.
KANISA LIJITATHMINI KABLA YA KUIHUKUMU JAMII
Kwa msisitizo mkubwa, waumini wanakumbusha mafundisho ya Injili yanayotaka Kanisa kujirekebisha lenyewe kwanza kabla ya kuikosoa jamii au Taifa.
ananukuu wazi Mathayo 7:3–5 kuhusu kuondoa “boriti” katika jicho la mtu mwenyewe kabla ya kuondoa “kibanzi” katika jicho la mwingine.
Hoja hii, kwa mujibu wa tafakuri hiyo, ndiyo msingi wa maadili unaolipa Kanisa uhalali wa kusema dhidi ya maovu ya dunia.
HOJA ZA SIASA ZACHOCHEA MGOGORO
Tafakuri hiyo pia inaibua hoja nzito kuhusu kuingizwa kwa Kanisa katika siasa za vyama, ikionya kuwa hatua hiyo:
• Huwagawa waumini
• Huporomosha mamlaka ya kimaadili ya Kanisa
• Huhatarisha umoja wa Kanisa na Taifa
Kwa mantiki hiyo, waumini wanasema hatua za viongozi wa kanisa kujihusisha au kuonekana kujihusisha na siasa za vyama ni kosa linalopaswa kutafakariwa na kurekebishwa haraka.
*AUNGA MKONO UCHUNGUZI WA VATICAN
Katika kile kinachoonekana kama msimamo unaozidi kuimarika, waumini wanaunga mkono hatua ya kuandikiwa Barozi wa Vatican nchini Tanzania kuomba uchunguzi wa mwenendo wa Padri Dkt. Charles Kitima, wakisisitiza kuwa hatua hiyo:
• Iko ndani ya Canon Law
• Inalenga kulinda heshima ya Kanisa
• Si uasi bali ni uwajibikaji
WASISITIZA KANISA SI PADRI, SI ASKOFU
Tafakuri hiyo inahitimisha kwa ujumbe mzito kwa uongozi wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania kwamba mamlaka ya kiroho ni huduma, si utawala, na kwamba Kanisa litasimama kwa ukweli, si kwa hofu.
“Kulilinda Kanisa ni kulinda ukweli, si kulinda makosa ya mtu,” waumini wanasema, wakikumbusha kuwa mwili wa Kristo una viu
ngo vingi, na kila muumini ana haki na wajibu wa kulilinda Kanisa lake.



0 Comments