'NDOA' ya mjukuu wangu Marcio Maximo na Vijana wa Kinondoni KMC kwa sasa inashikiliwa na uzi mwembamba kama ule wa mdudu aitwae buibui.Ni uzi mwembamba ambao hata mbu akithubutu kutua utahitimisha safari ya miezi michache ya ndoa hiyo.
Safari ya wanandoa hao imeshindwa kutimiza hata miezi sita tangu ndoa ifungwe kwa shangwe na vigelegele vingi.
Hakuna kinachoweza kunusuru ndoa hiyo isivunjike kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo katika Ligi Kuu Tanzania Bara.Hali ilivyo ni kama zimesalia dakika kama siyo sekunde uzi huo utakatika na wawili hao kutalikiana rasmi.
Bila shaka mwenyewe Maximo wakati huu atakua ameshakusanya mabegi ya nguo zake na kuyasogeza mlangoni kujiandaa na safari ya kurudi kwao Brazil kutokana na mambo kumuendea kombo.
KMC imegeuzwa jamvi la wageni kwenye Ligi Kuu licha ya uwekezaji mbalimbali iliyofanya katika timu hiyo.
Mashabiki wa timu hiyo wameshaikatia tamaa ya kubaki Ligi Kuu kama itaendelea kuwa chini ya Maximo.
Hawaoni dalili kama ana miujiza mipya ya kuitoa ilipo na kuipeleka nchi ya ahadi waliyokuwa wanaiota wakati Kocha huyo anatambulishwa.Hatua ya kwanza ya kuonesha hisia zao wamesusa kujitokeza kwenye mechi za timu hiyo wakati msimu uliopita walikuwa nyuma yake.
Maximo ameshindwa kuionjesha KMC utamu wa ushindi katika Ligi Kuu kiasi cha kuifanya timu hiyo kushikilia mkia.
Zipo tetesi KMC wameshaanza mazungumzo na Meck Mexime kujaribu kumuomba achukue mikoba ya Maximo.
Hili linakoleza uzito wa hoja kwamba Maximo na KMC zimesalia sekunde kabla hatujashuhudia talaka ikiwekwa mtandaoni kwamba ndoa ya wawili hao imevunjika kwa makubaliano ya pande mbili.
Kionambali M.Kionambali
P.O.BOX 2785
Kisiju/Mkuranga/Pwani
------------------------------
0 Comments