MBETTO:SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA NDIYO HITAJI LA WAZANZIBAR
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kinaamini kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ndiyo suluhisho la mahitaji ya wananchi.
Amesema kuwa chama hicho bado kinakusubiri chama cha ACT-Wazalendo ili kiungane nacho kuendelea kuunda Serikali hiyo kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar.
Ameeleza kuwa CCM kipo tayari kushirikiana na vyama vingine kwa ajili ya masilahi mapana ya Zanzibar na Watanzania wote, na kwamba ushirikiano huo unazingatia kikamilifu Katiba na sheria za nchi.
Aidha, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar siku zote imekuwa ikihamasisha amani na utulivu, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi unaoiwezesha Serikali kutafuta rasilimali na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Ameongeza kuwa kipaumbele kikubwa katika Ilani ya CCM ni amani, kwani ndiyo inayowezesha kuimarika kwa miundombinu ya maendeleo kama vile viwanja vya ndege, barabara, pamoja na miradi mingine ikiwemo maghala makubwa ya kuhifadhi chakula.
Kwa upande mwingine, amesema chama hicho kimeweka vipaumbele mbalimbali vinavyoendelea kutekelezwa kwa sasa, ikiwemo sekta za elimu na afya, kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi.
0 Comments