Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mitambo ya kuchakata na kuongeza thamani mazao ya kilimo, ikiwemo Mtambo mdogo wa kuzalisha sukari ulipo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu unaotarajiwa kuanza kufanya kazi Machi 2026 kwa lengo la kuchochea uzalishaji na kuongeza kipato kwa wakulima wadogo.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Kilimo, Bw. Gerald Mweli Oktoba 20, 2025, baada ya kutembelea karakana
ya uzalishaji mitambo katika Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo
Tanzania (TEMDO) iliyotengeneza Mtambo huo kwa lengo la kuona ni jinsi
gani Wizara yake inaweza kushirikiana na Shirika hilo katika kuwawezesha
Wanawake na Vijana walio chini ya Programu ya Kujenga Kesho iliyo bora.
Aidha,
Bw. Mweli amesema Wizara yake pamoja na taasisi zilizochini yake
zitaendelea kushirikiana na TEMDO kwa kutumia mitambo mbalimbali ya
kuongeza thamani mazao ikiwemo Mtambo mdogo wa kuzalisha sukari wenye
uwezo wa kuzalisha Tani 20 kwa siku ili kutimiza Malengo ya Serikali ya
Awamu ya Sita katika kuongeza ajira na kipato kupitia Kilimo.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TEMDO, Profesa Frederick Kahimba, na
Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini
(CAMARTEC) wamesema Taasisi zao ziko tayari kushirikiana na Wizara ya
Kilimo na Taasisi zake kwa kutengeneza mitambo yoyote itakayohitajika
pamoja na kutoa ushauri wakitaalamu na matengenezo ya mitambo pale
yanapohitajika
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa
Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Bi Irene Mlola, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya
Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), Bw. Patrick M. Mongella pamoja na
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Bw. Primus Kimaryo,
wameahidi kuendelea kushirikiana na TEMDO katika kuendeleza teknolojia
za viwanda vinavyolenga kuwasaidia wakulima kuongeza tija.
Vilevile,
Mkurugenzi wa usanifu na utafiti wa TEMDO Mhandisi Nicas Bernard
amesema kuwa anaona Faraja Taasisi yake ikifanikiwa kutatua changamoto
mbalimbali kwa kutumia ubunifu na teknolojia kwa kutengeneza mitambo
kulingana na mahitaji ya Wateja.
Tags
Habari



