Jamii za Kitanzania zimesisitizwa kuheshimu, kulinda na kurithisha mila na desturi zao pamoja na kuzingatia maadili ya Taifa yanayoambatana na upendo, amani, utulivu na mshikamano nchini.
Hayo yameelezwa na
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Amos Makala Oktoba 20, 2025 wakati
akifungua sherehe za kiutamaduni za rika la vijana wa jamii ya Maasai
wa Mkoa huo na Manyara zilizofanyika katika Boma Maalumu eneo la
Arumeru.
Katika sherehe hizo, Vijana wa Mkoa wa Arusha, Manyara
na Mikoa mingine nchini hukusanyika katika eneo maalumu ikiambatana na
vijana hao kupewa baraka na kufanyiwa tambiko maalumu ikiwa ni uzinduzi
rasmi wa msimu wa tohara kwa vijana hao utakaodumu kwa miaka saba
(2025-2032).
Mhe. Makala alisema, kuna umuhimu wa kuendeleza
mila hizo ili utamaduni wa Mtanzania uendelee kuwa hai na kurithishwa
kutoka vizazi hadi vizazi.
"Watanzania tunapaswa kulinda mila na
desturi zetu, ndio maana Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Dkt.
Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwa na dhamira ya dhati katika kukuza na
kuendeleza shughuli za Sekta ya Utamaduni na Sanaa kitaifa na kimataifa
pamoja na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata fursa ya kusherehekea na
kurithisha mila na tamaduni zao" alisisitiza Mhe. Makala.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Mnata Resani alisema
Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kwa kusheheni utajiri wa uanuwai wa
urithi wa utamaduni usioshikika uliofumbatwa katika lugha za asili kama
kibebeo cha urithi, mila na desturi, matambiko na sherehe za kijadi,
Sanaa na muziki wa asili, ngoma, majigambo, nyimbo, soga, utani, kazi za
mikono za kiutamaduni, maarifa na ujuzi wa asili ambao jamii inapaswa
kuuenzi na kuendelea kurithisha kwa manufaa ya vizazi vya sasa na
vijavyo.
Tags
Habari




