MKUU WA MKOA IRINGA ATAJA NGUZO ZA JESHI LA POLISI

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, ameitaka Jeshi la Polisi kuendeleza nidhamu, maadili na utu kazini, akisisitiza kuwa wanaowasimamia ni binadamu wenye mapungufu na hivyo wanapaswa kutendewa kwa haki na busara.

Akizungumza katika Uwanja wa Field Force Unit (FFU) wakati wa kilele cha maadhimisho ya Police Family Day, Mhe. Kheri amesema nidhamu ndiyo msingi wa ufanisi wa Jeshi la Polisi na daraja la kujenga imani ya wananchi kwa chombo hicho muhimu cha ulinzi na usalama.

Katika hafla hiyo, Jeshi la Polisi liliwatunuku vyeti vya pongezi na zawadi askari na wakaguzi waliofanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao kwa mwaka 2025. Mhe. Kheri amesema hatua hiyo ni chachu ya kuongeza bidii, ushindani chanya na uwajibikaji ndani ya Jeshi.

Maadhimisho ya Police Family Day yalianza rasmi Januari 10, 2025, yakihusisha michezo na shughuli mbalimbali zilizowashirikisha wananchi, hususan vijana, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mahusiano kati ya Polisi na jamii.






Post a Comment

0 Comments