TAFAKURI YA JUMAMOSI
- *Kanisa linapojipa uhuru wa kuikosoa Serikali, linawajibika pia kusikiliza na kuvumilia sauti za waumini wake vinginevyo haki hugeuka kuwa unafiki*.
Na. Godwin Jickson, Muumini Kanisa Katoliki
*Tafakuri ya dhamiri ya Kanisa*
Tafakuri ya Jumamosi hii inalenga zaidi dhamiri ya Kanisa kuliko mjadala wa kisiasa.
Inalenga mtazamo wa haki, si upande wa chama; maadili ya kichungaji, si shambulio la mtu; na uthabiti wa Injili, si kelele za mitandao.
Kwa kipindi kirefu sasa, Kanisa Katoliki nchini limejikuta katikati ya mjadala mkali unaohusu uhuru wa kujieleza, haki ya kukosoa, na mipaka ya mamlaka ya kichungaji.
Mjadala huu umechochewa na majibu makali ya baadhi ya viongozi wa Kanisa dhidi ya waumini waliotoa maoni mbadala au ukosoaji waliotaka Padri Charles Kitima ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu (TEC) kulitengenisha baraza hilo na kanisa kwa ujumla katika mahusiano na CHADEMA
*Swali la msingi ni: Je, Kanisa linaweza kudai haki ya kuikosoa Serikali bila masharti, lakini likashindwa kuvumilia kukosolewa na waumini wake? Ikiwa jibu ni hapana, basi tunapaswa kukiri kwa unyenyekevu kwamba tumetumbukia katika unafiki wa haki hali ambayo Yesu aliionya waziwazi.*
*Uhuru wa Kuhoji ni haki ya wote au ya wachache?*
Kwa miaka mingi, viongozi wa Kanisa wamekuwa mstari wa mbele kusisitiza umuhimu wa uhuru wa kujieleza wanapokosoa Serikali, sera zake, au mwenendo wa kisiasa.
Hoja zao mara nyingi zimejengwa juu ya msingi wa haki za binadamu, maadili ya kijamii, na wajibu wa Kanisa kuwa *“sauti ya wasio na sauti”.*
Huu ni msimamo unaokubalika kimaadili na kikanisa.
Lakini tatizo linajitokeza pale kanuni hiyo hiyo inapokataliwa inapotumika ndani ya Kanisa lenyewe.
Waumini wanapouliza maswali, kuonya, au kukosoa mwenendo wa viongozi wao, majibu yanayojitokeza si hoja za kitheolojia au kikanuni, bali kejeli, dharau na matusi.
*Hapo ndipo haki inapopoteza uhalali wake.*
*Majibu yaliyogeuka kuwa dharau*
Katika hotuba na kauli za hadhara, Askofu Mkuu Ruwa’ichi amenukuliwa akiwajibu wakosoaji kwa lugha kali na kejeli ikiwa ni pamoja na kuwaita “Malofa”, “wapumbavu,” “wajinga,” “Wasaliti”, “Njaa Njaa”. “wasio na akili,” au kuwadhalilisha kwa maneno yanayopunguza hadhi yao kama waumini.
Haya hayakuwa majibu ya hoja kwa hoja; yalikuwa matusi ya mamlaka dhidi ya hoja za waumini wanaolitakia heri kanisa lao .
Tafakuri ya kikanisa inatulazimisha kuuliza:
*Je, lugha hii inaakisi roho ya Injili? Je, matusi na kejeli ni zana halali za kichungaji? Au ni ishara ya mamlaka yanayohofia kuulizwa maswali?*
*SHERIA YA KANISA (CANON LAWS ) INASEMAJE?
Sheria ya Kanisa Katoliki iko wazi kuhusu haki na wajibu wa waumini pamoja na mienendo inayotarajiwa kwa wachungaji wao:
*“•Canon 212 §3: Waumini wana haki, na wakati mwingine wajibu, wa kutoa maoni yao kwa wachungaji kuhusu mambo yanayohusu mema ya Kanisa kwa heshima, busara na ukweli”.*
Ifahamike kuwa haki hii si zawadi ya Askofu; ni haki ya kikanisa.
Aidha,
•Canon 220: Inakataza kudhuru heshima njema na sifa ya mtu. Lugha ya dharau, kejeli na matusi ni kinyume cha kifungu hiki.
Kadharika,
•Canon 384: Inamtaka Askofu awe mfano wa busara, kiasi na upendo wa kichungaji, akilinda umoja wa Kanisa.
Lugha kali inayogawa waumini inakiuka wajibu huu.
Kama ambavyo inaendelea zaidi
•Canon 1373 (kwa tahadhari): Inahusu kuchochea chuki au uasi dhidi ya mamlaka ya Kanisa.
Tafsiri sahihi inahitaji busara lakini ukosoaji wa heshima hauwezi kufasiriwa kama chuki.
Kwa msingi huu, hakuna Canon Law inayoruhusu matusi kama majibu.
*Ukosoaji hujibiwa kwa hoja, si kwa kudhalilisha.*
*MKANGANYIKO WA KICHUNGAJI NA SIASA*
Chanzo kingine cha mvutano ni wasiwasi wa waumini kuhusu mwenendo wa Padri Charles Kitima.
Baadhi ya waumini wanaona kuwa kiongozi huyo anachanganya majukwaa ya Kanisa na misimamo binafsi ya kisiasa, akihusishwa wazi na mitazamo ya CHADEMA.
Iwe mtu anakubaliana na tathmini hii au la, jambo la msingi ni kuwa: *wasiwasi huo una haki ya kusikilizwa.*
Kwa kuzingatia kuwa Kanisa, kiasili, ni mama na mwalimu hivyo linapochanganya ujumbe wa wokovu na ajenda za vyama, linafanya waumini wake wagawanyike, linapoteza hadhi ya upatanisho, na linaweka doa kwenye dhamira yake ya kiroho.
*Hili ndilo tamanio la waumini si uasi, bali ulinzi wa Kanisa.*
*ISEMAVYO BIBLIA KUHUSU LUGHA ZA MAMLAKA*
Maandiko Matakatifu yanatoa mwanga usio na shaka katika rejea mbalimbali za ki biblia.
Mfano:-
•“Neno lenu na liwe daima na neema.” (Wakolosai 4:6)
•“Heri wapatanishi.” (Mathayo 5:9)
•“Msihukumu, msije mkahukumiwa.” (Mathayo 7:1)
•“Kifo na uzima viko katika ulimi.” (Mithali 18:21)
*Lakini juu ya yote, Yesu anatupatia kioo cha kujitazama:*
“Kwa nini waona kibanzi kilicho katika jicho la nduguyo,
lakini huoni boriti iliyo katika jicho lako?” - Mathayo 7:3
*UZITO WA TAFAKURI*
Hapa ndipo tafakuri inakuwa nzito:
*tunawezaje kudai haki ya kukosoa Serikali, lakini tukashindwa kuvumilia kukosolewa na waumini? Huu ni mgongano wa maadili unaohitaji toba ya pamoja, si majibu ya hasira.*
*NGUVU YA KANISA NI KUSIKILIZA*
TAFAKURI hii inatueleza kuwa Kanisa lenye afya halihofii maswali, hoja wala mijadala inayoibuliwa sio tu na waumini hata jamii kwa ujumla
Historia ya Kanisa inaonyesha kuwa marekebisho (reforms) mengi yalianza kwa maswali magumu kutoka ndani.
- Ifahamike wazi kuwa kusikiliza si udhaifu ni nguvu ya kichungaji
- ieleweke wazi kuwa kukosolewa si kudharauliwa ni mwanga wa kujirekebisha.
Tafakuri inaona viongozi wanapojibu maswali kwa kejeli, wanatuma ujumbe hatari kwamba mamlaka hayawajibiki.
Hilo linazalisha hofu, ukimya wa kinafiki, na mgawanyiko yote ambayo ni kinyume cha Injili.
*USHAURI WA KICHUNGAJI*
Je, Kanisa linapaswa kuwa vipi?
Ili kurejesha uaminifu na umoja, Kanisa linapaswa kufanya ifuatavyo:
1.Kujenga utamaduni wa kusikiliza
Kuanzisha majukwaa ya mazungumzo ya heshima kati ya viongozi na waumini.
2.Kurejesha lugha ya Injili, kujibu hoja kwa neema, si kwa matusi. kwa busara, si kwa kejeli.
3. Kutenganisha wazi Kanisa na siasa za vyama, Kanisa libaki sauti ya dhamiri ya taifa, si jukwaa la chama.
4. Kuheshimu Canon Law kwa vitendo kutambua haki ya waumini (Canon 212 §3) na kulinda heshima yao (Canon 220).
5. Kujitathmini kabla ya kujitetea
Kabla ya kushambulia wakosoaji, viongozi wajitazame kwanza.
*Hitimisho: Haki isiyo na unyenyekevu hugeuka unafiki*
Tafakuri ya Jumamosi hii inatualika sote viongozi na waumini kurudi kwenye unyenyekevu wa Injili.
Haki ya kuikosoa Serikali ni halali; lakini haki hiyo hiyo lazima iheshimiwe ndani ya Kanisa.
Vinginevyo haki hugeuka kuwa silaha ya upande mmoja.
Kanisa ni la Kristo, si la mtu.
Kanisa ni waumini.
Na ukweli, kama Injili inavyotufundisha, hauogopi maswali.

1 Comments
Sio leo kanisa limepoteza hadhi na dhamira ya kiroho. Ni kwa Karne nyingi dini nyingi zimejiingiza ktk mambo ya ulimwengu huu yaani siasa, vita na hata kusabababisha vifo vya watu wengi Sana. Ukitaka kujua hilo chunguza vita vya 2 vya Dunia ambapo Dini nyingi zilituma waumini wao kushiriki ktk vita. Na Kila upande wa upinzani ulijipata ukiwaua waumini wenzao wa upande mwingine. Hata Baba wa Taifa aliwahi kulisema jambo kama hilo lilitokea pale (Ruanda nadhani) Hebu pia nenda YouTube tafuta: "kiongozi Bora ni yupi?" Utamsikia Nyerere akisimulua jambo la kutisha kabisa ambapo waumini wa kanisa la Roma walichinjana kinyama!!! Tena ndani ya kanisa.
ReplyDeleteNenda kwenye vita vya Ukraine: Magazeti kadha yamelipotiwa yakiwa na jumbe mbalimbali kutoka kwa viongozi mbalimbali wa kidini wakiunga mkono vita.
Kwa hivyo haishangazi kwamba Biblia inataja uhusiano wa dini au dini kujiingiza ktk mambo ya ulimwengu huu kuwa ni Uzinzi wa kiroho. Soma- Yakobo 4:4 inasema hivi:
"Enyi wazinzi, hamjui kuwa rafiki wa Dunia ni kuwa adui ya Mungu? Yeyote anayekuwa rafiki wa Dunia anajifanya mwenyewe kuwa adui ya Mungu"
Kwa upande mwingine Dini zibadilike. Badala ya kutegemea mifumo ya kisiasa za ulimwengu huu, wawanjengee waumini wao Imani yenye nguvu ktk Ufalme wa Mungu.kwanu Biblia ina ahadi za Mungu wa pekee wa kweli asiyeweza kusema uwongo.
Kwanza kabisa watu wote kutia ndani viongozi wa kidini-wanapaswa kuzitii Mamlaka zimewekwa na Mungu mwenyewe (Serikali) kama ilivyoanlishwa na MM/Mungu kwenye Waroma 13:1-3 kulingana na andiko hilo msitari wa 2. Mtu anayekuwa dhidi ya Serikali anakuwa dhidi ya mpango wa Mungu naye atajiletea Hukumu yeye mwenyewe.
Unaweza kutua kidogo Ili ujaribu kufikiria msitari huo: "Mungu hawaoni watu wanaokuwa dhidi ya Serikali kuwa wako dhidi ya Serikali. Bali anawaona wakiwa dhidi yake mwenyewe (MUNGU)
Pili: kwenye Methari 24:21 (NWT) Biblia inaonya hivi: "Mwanangu, mwogope Yehova na mfalme. Wala usishirikiane na waasi*"
Mbo ni mengi muda ni mchache. Ila kwa kifupi: UFALME WA MUNGU NDIO SULUHISHO PEKEE LA MATATIZO YOOOTE YA BINADAMU.
Soma- Mathayo 6:10 & Daniel 2:44
Uia ufalme huo wa MUNGU utaambatana na baraka nyingi kama vile:
{1} UTAONDOA KIFO (Ufunuo 21 4:4 & Isaya 25:8)
Isaya 35:5,6 UTAONDOA uremavu wa aina zote
Isaya 33:24 hskutakuwa kuumwa
Isaya 33 25 wazee watakuwa vijana na nguvu za ujana watarudishiwa
Isaya 32:16-18 Haki itatawala Dunia nzima
Zaburi ya 72:16 chakula kitafurika
Japo sisi tumezoea mafuriko ya ayoua watu lakini wakati huo tunaambiwa kutakuwa na mafuriko ya chakula
Pi hakutakuwa na umasikini Dunia nzima kwaaama watu wote tutakuwa na Makao mazuri na kazi yenye kuridhisha soma- Isaya 65:21-23
Lakini swali ni: Ni nani watakaopata baraka hizo? Jibu la Biblia:
Zaburi ya 37:9-11 pi 29,34 waadilifu au wanaotii na kufuata shauri la Mungu linalopatikana ktk Biblia. Hata wewe unayesoma ujumbe huu unaweza kuwa miongoni mwa watakaookoka ikiwa tu utafuata njia ya uadilifu ktk mambo yote kuringana na maoni ya Mungu. Barikiwa. Tusifuate mihemuko ya baadhi ya viongozi wa kidini wenye masrahi kibinafsi na mambo ya kisiasa.
*Au wale wanaodai mabadiliko.