WAZIRI MASAUNI ACHAGULIWA MAKAMU WA RAIS BARAZA LA MAZINGIRA UMOJA WA MATAIFA


 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA).


Hayo yamejiri katika mkutano wa saba wa Baraza hilo uliofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), jijini Nairobi nchini Kenya, Desemba 12, 2025.

Uchaguzi huo umefanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 18 ya Kanuni za Utendaji za UNEP inayotaka Baraza kumchagua Rais, Makamu wa Rais pamoja na mwandishi katika kikao cha mwisho cha mkutano wake.

Masauni amependekezwa na Kundi la Nchi za Afrika, ambalo kwa kuzingatia kanuni za mzunguko na uwakilishi wa kijiografia, limepewa nafasi mbili za Makamu wa Rais katika Ofisi ya Baraza hilo.

Uchaguzi wake umeidhinishwa bila kupingwa, hatua inayodhihirisha imani na heshima kubwa ya jumuiya ya kimataifa kwa uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu.

Post a Comment

0 Comments