UCHAMBUZI WA KIJASUSI: KUTEKWA KWA MIJI YA BUKAVU,UVIRA NA KALEMIE KONGO CHINI YA WAASI M23

Na LUGETE MUSSA LUGETE.


Tarehe 27/1/2025 Muungano wa waasi wa Kitutsi AFC chini ya Corneille Nangaa waliuteka mji wa Goma mkoa wa Kivu Kaskazini na maeneo yake muhimu ikiwemo uwanja wa ndege na huduma mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kiusalama. Waasi hao ambao ni muungano wa zaidi ya makundi matano yaani AFC,M23,Red Tabara na mengine. Madai yao ni kwamba serikali ya Kongo chini ya Felix Tshisekedi sio halali na Wana mpango wa kwenda Kinshasa kuchukua nchi.Zaidi ya watu 3000 wamepoteza maisha na zaidi ya watu laki 500,000 wamekimbia makazi yao hiyo ni kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa kupitia kitengo cha haki za binadamu 

Leo alfajiri waasi wa M23 wameuteka mji wa Bukavu, Kivu Kusini na wanasonga mbele kuelekea Uvira na Kalemie ziwa Tanganyika. Malengo ya waasi wa M23 kuiteka Uvira yana sura mbili kijasusi.

Mosi: Kuzuia Jeshi la Burundi kuingia Kongo kulisaidia Jeshi la Kongo (FARDC) kupambana na waasi wa M23. Ikumbukwe kwamba Jeshi la Burundi lina mkataba na serikali ya Kongo kutoa huduma za ulinzi na kupambana na waasi wa M23 ambao wanaungwa mkono na serikali ya Rwanda kwa sababu serikali ya Rwanda inawaunga mkono waasi wa Red Tabara ambao ni Watutsi wenye lengo la kuipindua serikali ya Burundi inayoongozwa na Chama cha CNDD-FDD ambacho kimejaa Wahutu. Hivyo Waasi wa M23 wanazuia askari wa Burundi kuingia Kongo na Wana lengo la kuivamia Burundi.

Pili: Waasi wa M23 wameungana na waasi wa Red Tabara wa Burundi ambao walishiriki kwenye jaribio la Mapinduzi ya Burundi Mwezi Mei 2015 chini ya Generali Godefroid Niyombale na Alexis Sinduhije. Ndio maana kwenye chaguzi kadhaa za Burundi serikali ya Rwanda imekuwa ikijaribu kumuunga mkono Agathon Rwasa .

Kitendo cha waasi wa M23 kuiteka Bukavu Kivu Kusini na maeneo ya Uvira na Kalemie hali ya usalama wa taifa letu pendwa Tanzania liko mashakani kwa sababu zifuatazo.

Mosi: Sababu za kiuchumi na biashara. Wote tunafahamu Kwamba Kuna njia ya biashara na usafirishaji kutoka Kalemie Kongo kwenda Mpulungu Zambia kupitia ziwa Tanganyika, Kalemie Kongo kwenda Bujumbura Burundi kupitia ziwa Tanganyika na Kalemie Kongo kwenda Kigoma mjini Tanzania kupitia ziwa Tanganyika. Hivyo kitendo cha waasi wa M23 kuushika mjira wa Bukavu Kivu Kusini ni hatari sana kwa uchumi wa watu wa Kigoma, hasa maboti ya watu wa Kibirizi Kigoma ambayo hupeleka mizigo Uvira, Bukavu na Kalemie Kongo kupitia ziwa Tanganyika. Hata Burundi wako hatarini. Mpaka sasa hivi biashara kutoka Kigoma kwenda Kongo kupitia ziwa Tanganyika imesinyaa kutokana na hali ya usalama Kongo.

Pili: Sababu za kiusalama na Intelijensia
Kwa miaka mingi Rwanda imejaribu kupanua njia za kuingia Kongo kupitia ziwa Tanganyika ndio maana serikali ya Rwanda imekuwa ikijaribu kuichukua Burundi bila mafanikio. Hivi karibuni Rais wa Burundi Generali Evarist Ndayishimiye aliwahutubia Wananchi wa Burundi waishio mipakani mwa Rwanda na kuwaambia kwamba vita iko mlangoni kwa sababu Rwanda imepeleka askari wengi kwenye mipaka yake na Burundi na pia Burundi imepeleka askari wengi kwenye mipaka yake na Rwanda hivyo hali ni mbaya sana kiusalama. Ikiwa Bukavu Kivu Kusini na maeneo yake muhimu ikiwemo Uvira na Kalemie yakiendelea Kuwa chini ya waasi wa M23 tunaweza kushuhudia ujambazi ziwa Tanganyika na maeneo ya Kigoma,Katavi na Rukwa, biashara haramu,Magendo na silaha kuingia nchini Tanzania.

Tatu: Vita kati ya Rwanda na Burundi yaani vita kati ya waasi wa M23 na serikali ya Burundi ni vita kamili kati ya Rwanda na Burundi ambapo kama taifa tunapaswa Kuwa makini kwa sababu tutaelemewa na mzigo mkubwa wa wakimbizi kutoka Kongo na Burundi.

Nne: Jumuia ya Afrika Mashariki iko hatarini kupoteza mwelekeo Kwa sababu Kongo aliomba kujiunga Jumuia ya Afrika Mashariki akiamini kwamba kupitia Jumuia hii anaweza kupata msaada wa kupambana na maadui zake ambao ni Rwanda na Uganda.Hata hivyo matarajio ya Kongo ni madogo ndani ya EAC hivyo tunapaswa kufikiri kwa kina kama kobe na kuona mbali kama tai huku tukiweka mbele maslahi mapana ya Taifa letu pendwa Tanzania kiuchumi, kisiasa, kiintelijensia na kiusalama. Uzalendo, Umoja wa mshikamano wa kitaifa ni muhimu katika kipindi hichi ambacho jirani zetu yaani Rwanda, Burundi na Kongo wapo kwenye tandawi na songombingo za kiusalama.

Tano: Lengo la Rwanda ni kuichukua Burundi ili aweka kibaraka wake ndani ya Burundi na kuongeza mtandao wa kutorosha madini ya Kongo kupitia Burundi na kuingia Rwanda kupitia mkoa wa Chibitoke Burundi. Kwa mujibu wa taarifa za kiintelijensia ni kwamba Rwanda ana wasiwasi na njia ya Rutshuru na Bunagana kwa sababu Uganda nae yupo hivyo anatafuta njia ya peke yake ya kuingia Kongo bila uhusika wa Uganda na njia rahisi ni kuidhibiti Burundi.

Historia ni Mwalimu mzuri sana ngoja tujikumbushe tarehe 25/7/1996 Mbabe wa vita nchini Burundi Pierre Buyoya alifanya mapinduzi ya kijeshi kwa mara ya pili baada ya kumpindua Rais Sylivestre Ntibantunganya , Buyoya alikuwa Mtutsi aliyeungwa mkono na Rwanda. Buyoya pia alihusika kwenye mkataba wa Lemera Kwa lengo la kuigawa Kongo. Katika Operesheni Banyamulenge mwaka 1996 baadhi ya askari wa Rwanda waliingia Kongo kupitia Burundi ili kumuondoa Madarakani Generali Joseph Desire Mobutu Sese Seku Kuku Ngendu Wa zabanga.

Wakati wa utawala wa Pierre Buyoya Tanzania tulipata madhira makubwa hasa wakazi wa mkoa wa Kigoma mfano Jeshi la Tanzania mwaka 1997-1998 liliwahi kuwahamisha Wananchi wa kata ya Kagunga kuanzia Rusolo mpaka Zashe na kuwapeleka nyumbani Mwamgongo. Kwa sababu Buyoya aliwaleta wahuni kutoka Rwanda na kuwakaribisha Burundi. Ujambazi, biashara haramu, wakimbizi na magendo yalizidi kwenye mipaka ya Tanzania na Burundi kupitia ziwa Tanganyika. Kulikuwa na mtandao wa majambazi wa Kitutsi kutoka Burundi ambao walikuwa wanashirikiana na Banyamulenge kutoka Kongo kuiba injini na nyavu za wavuvi ziwa Tanganyika. Kutoka Kagunga mpaka Kirando na Mgambo mwambao wa Ziwa Tanganyika wizi ulikuwa umeshamiri mpaka Jeshi la Tanzania likaongeza ulinzi wa majini. 

Hali ilikuwa nzuri mwaka 2000 kwenye makubaliano ya Arusha kuhusu mgogoro wa Burundi ambapo mwaka 2003 Rais wa Tanzania Hayati Benjamin William Mkapa alimuomba Buyoya kujiuzulu na kupelekea mkataba wa amani wa kubadilishana madaraka ambapo tulishuhudia Domitien Ndayizeye akiwa Rais wa mpito wa Burundi kutoka 2003_2005 na baadae Pierre Nkurunziza kutoka 2005 mpaka mwaka 2020 alipoaga dunia.

Kwa kile kinachoendelea nchini Kongo , Rwanda na Burundi kama taifa tunapaswa kuchukua tahadhari kimya kimya kulinda mipaka yetu na maslahi yetu kiuchumi, kisiasa, kiintelijensia na kiusalama.

Nini kifanyike kupambana na hii kadhia kwa sababu nyoka wenye sumu kali wako mlangoni kwetu.

Mosi: Vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania, Burundi,Kongo na Zambia ni muhimu kuimarisha ulinzi na usalama wa ziwa Tanganyika. Ushirikiano na mbinu za pamoja ni muhimu sana kwa sababu waasi wa M23 wataanza kutoza ushuru na kuweka viongozi wao kwenye maeneo ambayo tunapakana nayo.

Pili: Serikali ya Tanzania itoe msaada wa haraka kwa Burundi ili isije kuangukia mikononi mwa Rwanda. Kama mwaka 2015 Rais wa Burundi Hayati Pierre Nkurunziza alirejeshwa Madarakani kufuatia jaribio la Mapinduzi ya Burundi chini ya Generali Godefroid Niyombale ambayo yalikuwa yamedhaminiwa na Rwanda.

Tatu: Wafanyabiashara kutoka Tanzania hasa Kigoma Wanaofanya biashara na mataifa ya Kongo na Burundi wanapaswa kupewa elimu ya kutosha kwa sababu hali sio nzuri.

Nne: Ni muda muafaka wa kuwakata vichwa nyoka wenye sumu kali kutoka mataifa yanayohujumu ulinzi na usalama wa taifa letu pendwa Tanzania. 

Tano: Jumuia ya Afrika Mashariki ichukue hatua stahiki na maamuzi magumu kuhusu mgogoro wa Kongo.

Sita: Shirika la Ujasusi la Tanzania liongeze Maafisa Vipenyo mipaka ya Tanzania na Burundi,Kongo na Rwanda.

Saba: Ufanyike msako mkali kuwabaini Majasusi wa Rwanda waliojipenyeza hapa nchini Kwetu Tanzania. Kama Rwanda ilifikia hatua ya kupeleka Majasusi Afrika Kusini kwenda kumuua Generali Patrick Karegeya tarehe 31/12/2013 huenda Kuna majasusi wa Rwanda hapa nchini Kwetu Tanzania.

Hitimisho: Ulinzi na Usalama wa taifa letu pendwa Tanzania ni jukumu la kila Mtanzania. Kila Mtanzania ashiriki kwa kadri ya uwezo wake. Ukiona mtu humuelewi na ana nia mbaya na taifa letu pendwa Tanzania tafadhari piga namba 112 utoe taarifa makao makuu ya Jeshi la Polisi.

Wako Mtiifu katika ujenzi wa taifa letu pendwa Tanzania. Jivunie Kuwa Mtanzania na lipende taifa lako na jitolee kwenye ulinzi na usalama wa taifa lako.

SIGNED BY LUGETE MUSSA LUGETE.
THE GRAND MAESTER.
GURU OF PHILOSOPHY.
MASTER OF HISTORY.
GIANT OF THE AGE.
PAN AFRICANIST.
Kayonka Kikenke Kamasa Mwamgongo Kigoma.
0755988284.
15/2/2025.

Post a Comment

0 Comments