Ilikuwa Desemba 10 2022, miaka mitatu iliyopita, pale bara la Afrika lilipogubikwa na huzuni kubwa kufuatia taarifa za kifo cha mwanamuziki wake nyota, Mwanamama Elizabeth Muidikay maarufu kama Tshala Muana.
Tshala Muana alifariki dunia alfajiri ya Disemba 10, 2022 katika hospitali ya Cinquaintenaire iliyopo jijini Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Safari ya maisha yake ya miaka 64 duniani ilifikia ukomo hospitalini hapo kwa huzuni kubwa.
Changamoto ya maradhi ya upumuaji iliyomkabili kwa takribani wiki moja, ilitamatikana kwa uamuzi wa kunyang'anya roho ya kipenzi cha wengi Muana na hivyo kupelekea uwepo wa vilio kwa mashabiki wa muziki kila kona barani Afrika.
Kabla ya changamoto hiyo iliyoondoa uhai wake, Muana aliwahi kuripotiwa kuugua Kiharusi mwaka 2020, kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya sukari na shinikizo la damu kwa muda mrefu. Hata hivyo hali yake iliripotiwa kuimarika na kurejea kuwa njema.
Taarifa ya kifo chake ilitawala vyombo vingi vya habari Afrika na duniani kwa ujumla. "Mama wa Afrika amelala" "Malkia wa Mutuashi hayupo tena"... Media nyingi ziliripoti taarifa za kifo cha Muana kwa headlines zilizoonesha simanzi na huzuni kubwa.
Maisha ya Muana yamepitia mengi katika safari ya kujitafuta, kujipata, kuanguka, kuinuka na kisha kusonga mbele, bila kujali nyuma yake ilikuwa ya changamoto ipi. Kifo kimezima ndoto zake nyingi alizopanga lakini hakuwahi kuzifikia katika maisha yake.
Muana mzaliwa wa Machi 13, 1958 mjini Lubumbashi, ni Mtoto wa Bi Alphonsine Bambiwa na mumewe, Kanali Mudikay Amadeus aliyekuwa Mlinzi wa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Kongo DRC, Hayati Patrice Emille Lumumba.
Safari yake kimuziki ilianza akiwa binti mdogo, mtumbuizaji kwenye kikundi cha ngoma za asili za kabila la Luba linalopatikana huko Kasai nchini Kongo DRC. Ngoma hiyo maarufu iitwayo 'Mutuashi' hupigwa na kuchezwa na wanawake kwenye shughuli mbalimbali za kijamii nchini humo.
Umahiri wa kucheza 'Mutuashi' (traditional dance) ukamfanya Muana kutamani kuwa mwanamuziki mkubwa. Taratibu akaanza kujipenyeza kwenye bendi za chini ili kumsaidia kukuza kipaji chake, wakati huo akivutiwa na muziki wa rhumba zaidi.
Baada ya kupambana kwa muda mrefu, hatimaye Muana akaanza kujipata. Mikono salama ya waimbaji nyota wanaoheshimika nchini Kongo, M'pongo Love na A'Beti Masikini ikashiriki kumnoa katika vipindi tofauti tofauti kutokea kanisa la Kibembe huko Elizabethville.
Nyota ya Tshala Muana ikaanza kung'ara. Miaka ya 80 ikaanza kuwa ya mafanikio baada ya kuachia vibao mbalimbali vilivyompa umaarufu mkubwa, huku akionekana kuchuana vikali na Mwanamama Mbilia Bel aliyeonekana kuwa mshindani wake mkubwa wakati huo.
Wakati haya yakitokea, Muana aliripotiwa kuwa na mahusiano na mtu aliyeonekana kuwa nyuma yake kwenye kila kitu kimuziki. Namzungumzia Rai Ouedraogo, Promota wa muziki maarufu kutoka Burkina Faso.
Inaelezwa kuwa Rai na Muana walikutana kwa mara ya kwanza kwenye shughuli za muziki nchini Ivory Coast na kisha baadae kuanzisha mahusiano ya kimapenzi. Kwa kifupi nyuma ya mafanikio ya Muana kimuziki hususan miaka ya 80 mpaka 90, Rai alihusika pakubwa mno.
Nyota ya Muana ikazidi kung'ara barani Afrika na duniani kwa ujumla. Kila alichogusa kwenye muziki lilikuwa Lulu, sikiliza vibao vya "Nasi-Nabali" "Kokola", "Tshibola", "Malu", "Kizunguzungu", "Munanga", "Tshikombo", "Lekela Muadi" na vinginevyo utaamini hiki nisemacho.
Lakini si hayo tu, Muana akatumia fursa ya umaarufu wake pia kutangaza utamaduni wa kabila lake la 'Luba'. Akatunga na kuimba nyimbo nyingi kwa lugha ya Ki-luba na kufanikiwa sana kutangaza utamaduni wa kabila alilotokea.
Mtindo wake wa kusakata ngoma ya asili ya 'Mutuashi' ukawa maarufu sana. Muana akasimikwa kuwa "Malkia wa Mutuashi' na mashabiki wa muziki wake, lakini Serikali ya Rais Mobutu Sese Seko (wakati huo) ikamteua kuwa Balozi wa utamaduni wa Kasai kupitia kabila la Luba.
Kibao cha "Karibu Yangu" alichoimba kwa Kiswahili kikaonekana kumtangaza zaidi Muana nchini. "Karibu Yangu" ikapendwa na kila mtu. Wimbo ukaimbwa na watu wa kila rika kutokana mashairi yake mepesi kueleweka zaidi kuliko tungo zake nyingine.




Unihurumie, hurumie..
Nakulilia unipee...
Unipeleke kwa mama
Atatupatia Mali
Tufunge oh, Ndoa ya lote..
Mpenzi oh, mimi na wewe
Ndoa oh, Ndoa ya lote..
Karibu oh, Karibu yangu
C'est ca, c'est ca..!!
C'est ca, c'est ca..!!
Usinitese moyoni...
Naomba ooh, usinitesee..
Unipeleke kwa baba
Atatupatia mali
Tufunge ooh, Ndoa ya lote..
Mpenzi ooh, mimi na wewe
Ndoa ooh, Ndoa ya lote..
Karibu ooh, Karibu yangu




Kunogewa kwa tungo za Kiswahili kukapelekea Muana kutaka kuingia matatani. Bendi ya Zaita Musica Wana "Zuke Muselebende" iliyokuwa ikiongozwa na 'Supreme' Fred Ndala Kasheba ikatoa kibao kiitwacho "Dezo Dezo". Muana akavutiwa na kibao hicho na kuamua kukirekodi upya kinyume na utaratibu.
Jambo hilo likazua taharuki kubwa baada ya mtunzi wa wimbo huo Kasheba kuanza hatua za kumburuza mahakamani Muana kutokana na kuiba tungo yake hiyo. Hata hivyo suala hilo liliripotiwa kuzungumzwa nje mahakama na makubaliano yao kubaki kuwa Siri mpaka leo.
Muana ni zao la wanamuziki walionufaika na siasa za Kongo wakati wa utawala wa Rais Mobutu. Kuondoka kwa Mobutu madarakani na kuingia utawala mpya wa Rais Laurent Desire Kabila, kulichangia kuvuruga masuala yake ya muziki.
Utawala wa Kabila ukampelekea Muana kuzigeukia siasa za Kongo na kuupa muziki kisogo kwa muda. Mwaka 1999 wakati Kongo ikiangaika kutunga Katiba yake mpya, Muana akateuliwa kuwa Mjumbe katika bunge la Katiba la nchi hiyo.
Siasa zikamchukulia muda na kupelekea kukaa zaidi ya miaka 3 bila kutoa wimbo wowote, na hata aliporejea tena kwenye muziki mwaka 2002 na kutoa albamu yake ya 'Dinanga' na kisha mwaka 2006 kutoa albamu nyingine ya 'Mamu National' hakuweza kurudi kwenye ukali wake wa zamani.
Pamoja na ukali wake katika muziki, Muana pia alijawa na vituko ambavyo wakati mwingine vilionekana kumpa sifa mbaya. Kituko kinachokumbukwa na wengi ni pale alipoamua kufunua gauni lake na kuwaonesha 'kufuli' mashabiki wakati wa Tuzo maarufu za KORA zilizofanyika nchini Afrika Kusini mbele ya Rais Nelson Mandela.
Hata hivyo, kitendo hicho kiliwagawa watu katika mitazamo, huku wengine wakimuona amekosa heshima na kujidhalilisha mbele ya Rais Mandela, na wengine wakionesha kumtetea kuwa hana kosa lolote, alichokifanya ni sehemu ya sanaa kupitia muziki wake.
Ni miaka mitatu kamili imetimu hii leo tangu kufariki dunia kwa 'Malkia wa Mutuashi' Elizabeth Muidikay wa Amadeus maarufu kama Tshala Muana. Princess of Luba Tribe from Kasai,... Mzaliwa wa Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Kongo.
Kwa bahati mbaya, Muana hakujaaliwa kuacha mtoto, wala hakuwahi kuolewa. Vifo vya watoto wake wawili aliowazaa nyakati tofauti tofauti na kufariki dunia wangali wakiwa wachanga, viliua kabisa ndoto ya kupata mtoto tena katika maisha yake.
Mwili wake umelazwa kwenye makaburi ya watu mashuhuri pale "Necropolis Cemetery" jijini Kinshasa pembeni ya Tabu Ley, Vercky's Kiamuangana, Papa Wemba, Lutumba Simaro, General Defao, King Kester Emeneya Papa Ndombe, Lokassa ya Mbongo, na wengineo wengi.
Waswahili husema, rafiki wa kweli ni yule asiyekutupa kwenye dhiki na faraja. Urafiki wa Muana na Mutuashi umedhihirisha hilo. Wamelala pamoja pale Necropolis Cemetery, ndiyo maana baada ya kifo cha Muana hutokaa umsikie Mutuashi tena.!
0713 555 773
#Balozi...........



0 Comments