Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Daniel Sillo, ameongoza kikao kazi cha pamoja kati ya Bunge na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kilichofanyika leo, Desemba 15, 2025, katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kiliitishwa kwa lengo la kujadili na kutoa mwelekeo wa kitaalamu kuhusu maandalizi, utekelezaji na uratibu wa mafunzo ya wabunge yanayotarajiwa kufanyika katika Bunge la Ufalme wa Morocco.
Katika kikao hicho, Wabunge wamejadili kwa kina masuala mbalimbali yanayohusiana na ushirikiano wa kibunge na kidiplomasia, ikiwemo kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo wa wabunge pamoja na kuimarisha mahusiano ya muda mrefu kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ufalme wa Morocco.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Said Shaib Mussa, pamoja na Maafisa wengine Waandamizi kutoka wizara hiyo na Bunge, ambapo walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kutekeleza majukumu ya kibunge na diplomasia ya nchi.

0 Comments