Mazungumzo ya kina kati ya Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo na Dk Anders Pedersen, mtaalamu maarufu wa jenetiki ya miti na mmoja wa waanzilishi wa Tanzania Tree Seed Agency (TTSA), yamekuwa miongoni mwa matukio muhimu katika siku ya tatu ya kikao cha 25 cha African Forestry and Wildlife Commission (AFWC25), Desemba 3, 2025, jijini Banjul.
Wawili hao wamekutana kando ya kikao na kujadili
mustakabali wa upatikanaji wa mbegu bora za miti ikiwa ni nyenzo muhimu
katika juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha misitu
ya kibiashara na kuongeza uzalishaji wa malighafi za viwanda.
Akizungumzia
safari ya taasisi hiyo, Profesa Silayo amesema TTSA iliyoasisiwa miaka
ya 1990 ikijengwa juu ya tafiti na ushauri wa wataalamu, kwa sasa
imeimarishwa zaidi kupitia Kitengo cha Uzalishaji Mbegu za Miti TFS,
ambacho kinahakikisha upatikanaji wa mbegu zilizothibitishwa kisayansi
kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi.
“Mbegu bora ndiyo msingi wa
misitu imara. Bila chanzo cha kuaminika, hatuwezi kuwa na misitu
inayostahimili tabianchi na magonjwa. Misitu ya kesho inaanza na mbegu
nzuri leo, na mbegu hizo zinapatikana TFS, karibuni,” amesema Profesa
Silayo akiwahimiza wadau na wawekezaji kununua mbegu bora kutoka kwa
wakala huo.
Dk Anders, ambaye amekuwa mshauri wa muda mrefu
katika sekta ya mbegu Tanzania na Afrika Mashariki, amesema Afrika iko
kwenye nafasi adhimu ya kuongoza dunia katika mageuzi ya misitu endapo
itawekeza kikamilifu kwenye ubunifu wa kielimu na vyanzo vya mbegu
vilivyoboreshwa.
“Tulipoanzisha TTSA tuliona pengo kubwa la
upatikanaji wa mbegu bora. Leo mahitaji yameongezeka zaidi, lakini uwezo
wa kuzalisha suluhisho upo, hasa kupitia taasisi kama TFS,” amesema.
Mazungumzo
hayo yameibua tena umuhimu wa kuwekeza kwenye sayansi ya mbegu bora,
jambo ambalo linatajwa kuwa uti wa mgongo wa misitu inayohitajika
kukabiliana na changamoto za ardhi, viwanda vya mazao ya misitu na
mahitaji mapya ya kimataifa.

0 Comments