KIGOMA NA SIFA YA UCHAWI KILA KONA

KIGOMA NA SIFA YA UCHAWI KILA KONA


KWA zaidi ya wiki moja sasa babu yenu Mzee Kionambali nipo zangu Mkoani Kigoma.

Kigoma ni miongoni mwa mikoa yenye sifa kubwa ya 'uchawi'.

Kwa muda mrefu  tumekua tukiaminishwa Mkoa huu licha ya  kubarikiwa rasilimali mbalimbali lakini pia mojawapo ni hiyo ya uchawi kama ilivyo kule Sumbawanga Mkoani Rukwa.

Tunayoaminishwa tukiwa sehemu mbalimbali za nchi yetu au nje ni tofauti na Kigoma ninayojionea kwa sasa.

- Ni tofauti kabisa. Ni kama kuna Kigoma mbili. Kuna ile unayoisikia ni tofauti na hii ninayoiona. Ni mbili tofauti.

- Kigoma unayoisikia ni ile inayosifika kwa uchawi. Ni uchawi. Uchawi. Uchawi uliopitiliza.

°Kwa namna fulani hofu hiyo iliicheleweshea Kigoma maendeleo  watu kushindwa kuja kuwekeza fursa za kiuchumi.

Nina kundi kubwa la marafiki zangu wenye ukwasi ukiwashawishi waje Kigoma kuwekeza  unaweza kugombana nao.
Imani potofu imeiteka akili yao. Siwalaumu.

- Kigoma niliyokutana nayo ni tofauti. Kiufupi tunaikosea sana Kigoma na watu wake. Tunawakosea sana.

 Mengi tunayoaminishana tukiwa makwetu ni tofauti na hali halisi ya hapa ilivyo. Tofauti kabisa.

- Wanasema ni ngumu kuuona uchawi kama wewe sio mchawi, lakini Kigoma haiko  tunavyoaminishana.
 Iko poa na watu wake wanafanya kazi zao kama kawaida. 

 - Hapa niliposimama na sehemu nyingine sijapishana na mabibi wala mababu. 

Napishana na vijana wachakarikaji wanaokimbizana na mkate wao wa kila siku.
Nimejaribu hata kupiga vifuu teke barabarani labda ntavimba mguu lakini wapi.Mambo ni tofauti kabisa.

- Kigoma kulivyo ni kama sehemu nyingine. Pia kitendo cha kupakana na boda za kwenda nchi za Burundi, Zambia na Congo imeufanya mji  kuchangamka kibiashara.
Nawaza tu mara SGR itakapoanza safari za kuja Kigoma na pia kukamilika kwa bandari ya kisasa inayojengwa na serikali.

Siku chache za uwepo wangu hapa nimegundua hata upatikanaji wa pesa ni mkubwa mno kwa sasa.

Nyumba za zamani enzi za ukoloni zimeanza kupotea na maghorofa yanaota kila kukicha.

Karibu maeneo ya Ujiji, Mwanga,Buzebazeba na kwingineno ujionee.

Barabara za lami  nimekutana nazo kila kona lakini sijakutana na uchawi wala wachawi.

 Kuna mzunguko sana na pesa hapa. Mazingira ya watu kufanya kazi bila kuchoka imeufanya mji kuwa na fursa nyingi za kujipatia pesa.

Nawashangaa hata vijana wanaokimbilia Dar es Salaam na kuacha fursa kubwa mkoani kwao.

- Kuna mikoa mingi nchini haina sifa za Kigoma. 
- Ni hivyo tu tumeamua kuipakazia sifa wasiyo nayo na wenyewe hawapendi jinsi tunavyowaona kama wana mambo ya kishirikina. Jambo hili linawakera. 

Kinachonifurahisha hapa saa moja jioni bado jua halijazama.Ingekua mwezi wa Ramadhani yangekua mateso makubwa kwa siye wafungaji.

 -Lakini kubwa lingine hapa Kigoma kuna baridi. Binafsi sijui kama leo asubuhi nilikoga au nilinawa miguu. Sijui! 

  - Baridi ni wastani licha ya jua kuchomoza.Wakati Dar es Salaam nyuzi joto ikiwa 30 hapa nyuzi joto ni 27 kwa nyakati za mchana na usiku nyuzi joto 21.

- Hii inaashiria hapa kuna baridi kali jioni.
- Kwa wazee kama miye hali ya hewa ya baridi kidogo inatusumbua hasa ukizingatia niko mbali na bibi yenu.

Kionambali M.Kionambali

S.L.P 2785

Ujiji/Kigoma

0754-629298

 

Post a Comment

0 Comments